Habari Mseto

Wahudumu wa afya 905 wapatwa na corona

September 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WINNIE ATIENO

WAHUDUMU wa afya 905 wameathiriwa na ugonjwa wa Covid-19, takwimu kutoka wizara ya Afya zinaonyesha.

Haya yanajiri huku serikali ikikabiliana na tishio la maambukizi ya virusi vya corona miongoni mwa wahudumu wao wa afya, jambo linalozua taharuki kwa jamii.

Hata hivyo, mkuu wa idara ya afya ya umma katika wizara hiyo, Bi Susan Mutua, alisema serikali inajitahidi kukabiliana na tishio la maambukizi miongoni mwa wahudumu wa afya, kwa kuweka mikakati ikiwemo mafunzo na uhamasisho.

Akiongea kwenye uzinduzi wa mafunzo na uhamasisho wa wahudumu wa afya katika kaunti 10 nchini, Bi Mutua alisema serikali itahakikisha wahudumu hao wa afya wanalindwa ili kuepuka maambukizi ya virusi hivyo ili wawe vielelezo bora.

“Katika kila kaunti 10 tunazozilenga, tutawapa wahudumu 400 wa afya mafunzo na uhamasisho wa namna ya kudhibiti maambukizi, kujilinda dhidi ya virusi vya corona na namna ya kubadili tabia wakati tunapopambana na janga hili. Hatutaki wahudumu wetu wa afya wafariki kutokana na janga hili ni sharti tuwalinde,” alisema Bi Mutua.

Kaunti zinazolengwa ni zile zilizoathiriwa zaidi na Corona; zikiwemo Mombasa, Kwale, Nairobi, Meru, Embu, Kisii, Homabay, Migori, Siaya na Kakamega.Aliwasihi Wakenya wasilegeze juhudi za kutekeleza masharti ya kupambana na janga hilo.

Bi Mutua aliwasihi wahudumu wa afya wa nyanjani kuwasaka wale wanaoathirika na maradhi hayo na kuwapa rufaa hospitalini ili wapate matibabu mapema.

“Hatufai kuogopa Covid-19, ukipimwa na kupatikana na virusi utapewa matibabu hata nyumbani kwako. Tuendelee kuvaa barakoa na kuosha mikono kila mara ndio njia pekee ya kuepuka maambukizi,” alisema Bi Mutua.

Jana serikali ilitangaza kwamba kuna matumaini huenda nchi ikafanikiwa kudhibiti msambao wa corona.

Akizungumza mjini Bomet, Waziri Msaidizi wa Afya, Dkt Rashid Aman alisema iwapo maambukizi yataendelea kupungua katika wiki mbili zijazo, huenda serikali ikafikiria kulegeza baadhi ya masharti.

Idadi ya watu 179 walioambukizwa ni ndogo, ikilinganishwa na mwezi mmoja uliopita ambapo karibu watu 800 walikuwa wakitangazwa kwa siku.

“Iwapo kila mtu atawajibika, na serikali za kaunti zitaunga mkono juhudi hizi, basi bila shaka tutafanikiwa kuangamiza Corona hapa nchini,” akasema.