BBI: Vigogo sasa waelekeza zana zao makanisani
Na WANDERI KAMAU
VIGOGO wa kisiasa nchini sasa wameanza kukimbilia makanisani kutafuta uungwaji mkono kwenye misimamo yao kinzani kuhusu ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) na uchaguzi mkuu wa 2022.
Ni mbinu wanayoonekana kutumia Rais Uhuru Kenyatta, Naibu Rais William Ruto, kiongozi wa ODM, Raila Odinga, Seneta Gideon Moi (Baringo) kati ya vigogo wengine kwenye juhudi za “kuwateka” ili kuunga mkono miegemeo yao.
Jumapili iliyopita, Dkt Ruto alirudi kanisani kwa kishindo, alipohudhuria ibada katika Kanisa la AIC Pipeline, eneobunge la Embakasi Kusini, jijini Nairobi.
Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Dkt Ruto kuhudhuria ibada yoyote kwa karibu miezi sita, tangu serikali ilipoyafunga makanisa mnamo Machi ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.
Kabla ya makanisa kufungwa, Dkt Ruto alikuwa akihudhuria ibada za maombi kila Jumapili katika maeneo kadhaa nchini, huku akitumia majukwaa hayo kuwajibu washindani wake kisiasa.
Kwenye kipindi hicho cha miezi sita, Dkt Ruto amekuwa akishiriki ibada za maombi katika makazi yake ya Karen, kwa kukutana na jumbe za viongozi wa kidini kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Ingawa jumbe kutoka afisi yake zimekuwa zikieleza lengo kuu la ibada hizo ni “kuiombea nchi”, ‘Jamvi la Siasa’ limebaini kwamba Dkt Ruto analenga kuwarai viongozi hao kupinga mchakato wa BBI.
Hilo lilithibitishwa na hotuba yake Jumapili, aliposema kuwa mageuzi yoyote ya kikatiba yanapaswa kuzingatia matakwa ya wananchi, badala ya maslahi ya viongozi.
“Kwa wale ambao tumebahatika kupata nyadhifa za uongozi, tunapaswa kuyapa kipao mbele masuala yanayowaathiri wananchi, bali si sisi binafsi. Mageuzi yoyote ya kikatiba yanapaswa kusukumwa na wananchi,” akasema.
Kwa mujibu wa wadadisi wa siasa, hatua ya Dkt Ruto kutoa kauli hizo kwenye kanisa ni ishara kwamba hilo litakuwa jukwaa muhimu kwake kuendesha kampeni zake.
Wanasema hiyo ni ishara huo ndio ulikuwa “uzinduzi wa kampeni ya ‘La’ dhidi ya mchakato huo.”
“Dkt Ruto ameeleza wazi kuwa atapinga mchakato wa BBI, ikiwa hautazingatia maslahi ya wananchi. Hii haitakuwa mara yake ya kwanza kulitumia kanisa kwani alifanya hivyo mnamo 2010 alipoungana na viongozi wa kidini kuipinga Katiba ya sasa,” asema Bw Geoffrey Munyui, ambaye ni mdadisi wa siasa.
Mdadisi huyo anasema kuna ishara Dkt Ruto kutobadilisha msimamo wake, kwani juhudi zake pia zitakuwa kama njia ya “kulipiza kisasi” mageuzi ya kisiasa yaliyofanywa na Rais Kenyatta kwenye uongozi wa Chama cha Jubilee (JP), ambapo washirika wake wengi katika mrengo wa ‘Tangatanga’ walipoteza nyadhifa zao kwenye Seneti na Bunge la Kitaifa.
Baadhi ya wandani wake waliotolewa kwenye nyadhifa zao ni maseneta Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet) kama Kiongozi wa Wengi, Susan Kihika (Nakuru) kama Kiranja wa Wengi, Kindiki Kithure (Tharaka Nithi) kama Naibu Spika kati ya wengine.
MIGAWANYIKO
Licha ya juhudi hizo, wadadisi wameeleza kuna uwezekano migawanyiko mikubwa ikashuhudiwa kwenye makanisa, baada ya kuibuka kuwa kando na Dkt Ruto, Rais Kenyatta na Bw Odinga vile vile wanawarai baadhi ya viongozi kuwasaidia kuwafikia Wakenya zaidi kuunga mkono mpango.
Duru zimeeleza baadhi ya viongozi ambao wawili hao wanalenga kuwatumia ni Muungano wa Maaskofu wa Kanisa Katoliki Kenya (KCCB).
Mwishoni mwa Februari, maaskofu wakuu wa kanisa hilo walimtembelea Rais Kenyatta kwenye Ikulu na kumwahidi kuunga mkono BBI.
Ujumbe huo uliongozwa na Kadinali John Njue na Askofu Philip Anyolo wa Dayosisi ya Kisumu, ambaye pia ndiye mwenyekiti wa muungano huo.
“Tunawaomba wadau wote kuunga mkono mchakato huu muhimu na kusahau maslahi yao yote,” akasema Kadinali Njue.
Majuzi, Askofu Anyolo alisisitiza kuwa kanisa hilo bado halijabadilisha msimamo wake
.Mabwana Odinga na Moi nao wamekuwa wakikutana na jumbe mbalimbali za viongozi hao majumbani mwao, yote yakionekana kama hatua ya kuwarai kuunga mkono ripoti hiyo.
SAUTI
Licha ya juhudi hizo, wadadisi wanaonya kwamba kuna uwezekano kanisa likapoteza sauti yake na mwelekeo kuhusu mchakato huo muhimu, ikiwa halidhihirisha umoja.
Kwa mujibu wa Bw Gideon Kitheka, ambaye ni mdadisi wa siasa, viongozi wa kidini wanapaswa kutahadhari kupotoshwa na wanasiasa, kwani lengo lao ni kuendeleza maslahi yao.
“Viongozi wa kidini wanapaswa kujiuliza kuhusu sababu wameibukia kuwa ‘muhimu’ mara moja, ambapo kila kigogo wa kisiasa anataka kukutana nao. Lengo lao kuu ni kuwahonga ili kuwarai wafuasi wao kuunga mkono mchakato huo ili kujifaidi wao wenye,” akasema Bw Kitheka.
Mdadisi anasema mbinu iyo hiyo ndiyo walitumia Rais Kenyatta na Dkt Ruto mnamo 2013 kufanyia kampeni walipokabiliwa na mashtaka ya uhalifu wa kibinadamu katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).
Anasema kanisa linapaswa kudhihirisha msimamo thabiti kuhusu masuala yanayoiathiri nchi kama ilivyokuwa katika miaka ya themanini na tisini.
“Viongozi wa sasa wanapaswa kujifunza kutoka kwa watangulizi wao kama maaskofu Alexander Muge, Timothy Njoya, Manasses Kuria kati ya wengine kuzungumza kwa sauti moja kwa manufaa ya nchi,” akasema