TAHARIRI: Shule zisichelewe hadi mwaka ujao
Na MHARIRI
RIPOTI kuhusu hali ya maambukizi ya virusi vya corona nchini inaonyesha kupungua kusambaa kwa kiwango kikubwa.
Kwa mfano Jumapili, kutoka kwa vipimo 3,093 ni watu 83 pekee waliogunduliwa kuwa wameambukizwa.
Hii ni hatua kubwa ikilinganishwa na miezi miwili iliyopita, ambapo kwa siku watu walikuwa kwa wastani 600.
Serikali kwenye ripoti zake za kila siku vile vile imeonyesha kwamba watu wengi wanaendelea kupona wakiwa nyumbani, ikilinganishwa na wanaoponea hospitalini.
Baadhi ya watu waliowahi kusemekana kuambukizwa corona wanasema hata wanapowekwa karaantini au hospitalini, cha mno zaidi ni kutumia vyakula vyenye Vitamini C pamoja na kuota jua na kufanya mazoezi.
Kuendelea kupungua kwa visa hivi kwafaa kutoe fursa kwa waunda sera na viongozi kujadili uwezekano wa kufungua shule mapema kabla ya Januari 2021.
Waziri wa Elimu, Prof George Mahoga amekuwa akibadili kauli kila kukicha. Iwapo hatashauriwa, au Rais Uhuru Kenyatta kushauriwa kwamba kufungua shule ni muhimu, huenda Wakenya wakasubiri kwa muda mrefu watoto wao kurejelea masomo.
Katika mataifa ya Ulaya, watu wameanza kurejelea kucheza mpira. Ligi ya EPL inang’oa nanga Jumamosi huku ligi ya Mpira wa Vikapu (NBA) ikiendelea nchini Amerika.
Watoto kawaida ni watu wanaokimbia hapa na pale na si rahisi wao kukaa sehemu moja. Isitoshe, serikali ilitangaza kuwa itanyunyiza dawa katika shule zote kabla hazijaanza kupokea wanafunzi.
Kufunguliwa kwa shule kutasaidia kukwamua uchumi wetu ambao umesambaratishwa na janga la corona.
Shule ni wateja wakuu wa bidhaa za wakulima kama mahindi na maharagwe. Wauzaji mikate, wasambazaji kuni, wauzaji sare za shule na hata mafundi wa ujenzi hutegemea vibaruaa vyao kutoka kwa shule.
Iwapo zitafunguliwa, uchumi katika sekta hizo utaanza kupata uhai tena. Badala ya kuendelea kufunga shule wakati ambapo imebainika njia bora ya kujikinga na maradhi haya ni kuvaa barakoa na kunyunyiza dawa, basi tutaendelea kuathirika kama taifa.
Kama ambavyo serikali ilifungua miji ya Nairobi na Mombasa lakini ikabakisha kafyu usiku, inaweza kufungua shule na kuweka angalau mhudumu mmoja wa afya katika kila shule ili wafuatilie afya za watoto wakati tunapoendelea na masomo.