Wakazi wa Gatundu Kaskazini washauriwa kupanda macadamia
Na LAWRENCE ONGARO
UKUZAJI wa zao la macadamia umetajwa kama ‘dhahabu’ ambapo mkulima anaweza kupata hela nyingi za kumfaa.
Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina alikutana na wakulima 100 katika kijiji cha Kanyoni eneo la Gatundu Kaskazini huku akiwahimiza kuzamia katika kilimo cha macadamia.
“Leo nimefika hapa kijiji cha Kanyoni, Gatundu Kaskazini kwa lengo la kuwahamasisha wakulima eneo hili kukuza zao la macadamia,” alisema Bw Wainaina.
Alisema zao hilo lina faida tele kwani mkulima yeyote anayejituma kukuza zao hilo bila shaka “atafurahia matokeo ya mavuno yake kwa kupokea kitita cha maana.”
“Iwapo kila mkulima atajihusisha na ukuzaji wa macadamia, baada ya muda mchache ataridhika na mavuno yake kwa sababu yana soko la haraka,” alisema mbunge huyo.
Alieleza kuwa ifikapo mwaka wa 2022 Kenya inatarajiwa kuwa imepanda miche 10 milioni.
Alisema kwa mwaka wanastahili kupanda miche 200,000 ili kupata mazao ya kuleta faida kubwa.
Wakati wa mkutano huo wakulima hao walinufaika kwa kupokea mbolea aina ya Organic.
Wakulima hao pia walipata mafunzo jinsi ya kupanda macadamia na kutarajia kupata mazao mengi.
Mbunge huyo alisema baada ya kupata mavuno ya macadamia wakfu wa Jungle Foundation, litakuwa mstari wa mbele kuwatafutia soko katika nchi za nje.
“Nyinyi kama wakulima mtafaidika pakubwa wakati mazao yenu yatafika katika masoko ya nje. Kwa hivyo mjitahidi muwe wakulima wenye bidii,” alisema Bw Wainaina.
Alisema zao hilo tayari limeshamiri katika kaunti 10 za hapa nchini.
Katika eneo la mlima Kenya kuna kaunti saba zinazohusika na ukuzaji wa macadamia.
Kaunti zingine ni Taita Taveta, Trans Nzoia, na Baringo.
Alisema zao hilo linastahili kuuzwa kwa bei ya Sh70 kwa kilo moja.
Mkulima Paul Kahiga Ngaruiya alisema katika kijiji hicho cha Kanyoni wakulima wengi wamegeuza mawazo yao kwa ukuzaji wa macadamia hata ingawa zao kuu katika eneo hilo ni chai na mananasi.
“Tayari vijana wengi wameanza kukuza zao hilo kwa sababu wamejionea umuhimu wake. Wengi wao maisha yao yameimarika,” alisema Bw Ngaruiya.
Alisema wanafuata maagizo yote waliopewa na mbunge huyo kuhusu ukuzaji wa macadamia.
Mkulima mwingine, Leah Wanjiru Mwangi anayekuza sana majanichai alisema ataanza kukuza zao hilo ili ajiongezee mapato ya kifedha.
“Sisi wakulima wa majanichai katika eneo hili tumefurahia kupewa mafunzo na Bw Wainaina ambaye ametuhamasisha umuhimu wa kuvuna mazao mengi kupitia macadamia,” alisema Bi Mwangi.