• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 10:50 AM
Wabunge wamshauri Ruto aanze misururu ya kampeni ya kuwania urais

Wabunge wamshauri Ruto aanze misururu ya kampeni ya kuwania urais

Na SAMMY WAWERU

BAADHI ya wabunge wa kundi la ‘Tangatanga’ wamemtaka Naibu Rais William Ruto aanze kufanya kampeni ya kumrithi Rais Uhuru Kenyatta 2022.

Kutokana na matukio ya hivi punde, ambapo baadhi ya mwaziri wameonekana kumshambulia Dkt Ruto hadharani huku wakizungumza kuhusu urithi wa Ikulu, wabunge hao wamesema hawaoni haja tena ya Naibu Rais kusubiri kuanza kampeni.

Wakiongozwa na mbunge wa Mathira, Nyeri, Rigathi Gachagua, wamemshauri Bw Ruto kuanza kufanya kampeni za 2022 waziwazi, wakihoji hatua hiyo ‘imechochewa na mawaziri hao ambao wamekuwa vibaraka wa kundi la Kieleweke na kugeuza nyadhifa zao kuwa uga wa siasa’.

Makundi ya ‘Tangatanga’ na ‘Kieleweke’, yaliibuka baada ya Handisheki kati ya Rais Uhuru Kentatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga, Machi 2018.

Kwenye ziara ya Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i eneo la Kati wiki iliyopita kukagua miradi ya maendeleo, akiandamana na Waziri wa Afya Mutahi Kagwe, Bw Kagwe alisema Dkt Matiang’i pia ametosha kuwa Rais.

Naye Waziri wa Mazingira na Misitu Keriako Tobiko alimcharura Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen, akimtaja Dkt Ruto kama ‘karani’ wa Rais Kenyatta. Ni matamshi ambayo hayajapokelewa vyema, hasa katika kundi la Tantatanga linaloegemea upande wa Naibu Rais.

“Ninamsihi Naibu Rais aache Rais na mawaziri wake wafanye kazi. Ajitose kwenye uga wa kampeni atafute kura za urais 2022,” akasema Bw Rigathi.

Akionekana kuwajibu wanaomshambulia Naibu Rais na kupigia debe Dkt Mating’i awe rais 2022, mbunge huyo alisema Waziri huyo wa Usalama wa Ndani anapaswa kujua Dkt Ruto alichaguliwa na wananchi na Matiang’i kuteuliwa na Rais.

“Matiang’i anadhani atatumia machifu na wakuu wa polisi achaguliwe kwa nguvu? Tumeona kuna wanaotaka awe rais na Kagwe, Waziri Mkuu. Mawaziri hao wajue Ruto alichaguliwa na umma, wao wameteuliwa. Wao ndio makarani. Hata hivyo, Dkt Ruto ni karani wa mahastla,” Bw Rigathi akasema.

“Mawaziri wa Rais Uhuru ndio wameanza siasa. Wanaume ni kuonana, hata sisi sasa tutatokea,” mbunge huyo akasema. Rigathi alisema hayo Jumapili usiku, kwenye mahojiano na runinga ya Inooro, inayopeperusha matangazo yake kwa lugha ya Kikuyu.

Wakati huo huo, Naibu Rais Jumapili mchana baada ya kuhudhuria ibada ya kanisa eneo la Athi River, Machakos, alihutubia umati wa watu, huku akiwataka mawaziri wanaomshambulia kwa maneno kufanya kazi waliyopewa.

Dkt Ruto alisema wajikakamue kutekeleza na kaufikia Ajenda Nne Kuu za Rais, akisema kipindi cha siasa bado hakijawadia.

You can share this post!

Orlando Pirates ya Afrika Kusini pazuri zaidi...

COVID-19: Kenya yathibitisha visa vipya 102