• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Safaricom yatoa msaada wa vifaa vya PPE katika hospitali ya Thika Level 5

Safaricom yatoa msaada wa vifaa vya PPE katika hospitali ya Thika Level 5

Na LAWRENCE ONGARO

SAFARICOM Foundation imetoa msaada wa vifaa vya hospitali kwa Thika Level 5, kwa lengo la kukabiliana na Covid-19.

Gavana wa Kaunti ya Kiambu Dkt James Nyoro, alisema hatua hiyo ya kampuni ya Safaricom ni ya kupongezwa kwa sababu hiyo ni njia moja ya kukabiliana na Covid-19.

“Madaktari na wauguzi wa hospitali ya Thika Level 5, watapata afueni kwa sababu watapokea nguo maalum za PPE ili waweze kufanya kazi yao bila vikwazo. Tunajua wamekuwa na wakati mgumu wanapoendesha kazi yao katika hospitali,” alisema Dkt Nyoro.

Alitaja msaada huo kama wa kupongezwa kwa sababu kampuni hiyo imetoa msaada wa thamani ya Sh2.7 milioni.

Aliwahimiza wananchi popote walipo waendelee kufuata maagizo yote ya Wizara ya Afya ili kukabiliana na janga hilo la corona.

“Hata ingawa maradhi ya corona maambukizi yanaonekana ni kama yanapungua kiasi, lakini wananchi hawastahili kulegeza kamba. Tuendelee kujikinga kama kawaida,” alisema Dkt Nyoro.

Alisema hospitali ya Tigoni ambayo ilikuwa na wagonjwa wa Covid-19 waliokuwa wamelazwa huko sasa wamebaki wachache wanaougua maradhi ya Covid-19.

Kuhusu usimamizi wa kaunti hiyo alisema wamepitia masaibu mengi kwa sababu  wanapitia wakati mgumu kifedha.

“Tayari tumelipa mshahara wa mwezi Julai, lakini mwezi Agosti bado. Tunawaomba maseneta wafanye jambo la busara ili wapitishe mswada wa mgao wa fedha zinazopelekwa katika kaunti,” alisema gavana huyo.

Alisema iwapo kwa muda wa wiki mbili hakutakuwa na dalili zozote za kupata pesa kutoka kwa serikali kuu, bila shaka itawalazimu kusitisha shughuli zote zinazoendeshwa katika kaunti zote.

Aliwahimiza wafanyakazi wote wafanye kazi kwa bidii ili kufanikisha malengo ya kaunti hiyo ya kutumikia wananchi bila ubaguzi.

You can share this post!

COVID-19: Wizara kutoa mwongozo mpya wa mazishi

FKF yatoa ratiba ya uhamisho wa wachezaji katika ligi ndogo