• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:38 AM
Fundi wa majahazi anayeunda mashua na mitumbwi

Fundi wa majahazi anayeunda mashua na mitumbwi

Na DIANA MUTHEU

NI mwendo wa saa saba mchana na wavuvi wamekwisha kuondoka kutoka katika eneo la uvuvi (BMU) la Ngare lililo katika mkondo wa maji ya bahari Hindi wa Port Reitz, kaunti ya Mombasa na kuwaacha vijana wadogo wakiogelea.

Kwa Ali Juma, huu ndio wakati mwafaka wa kutilia maanani mradi wake mkubwa.

Katika mradi huu ambapo anatengeneza jahazi lenye urefu wa mita moja na upana wa mita nne, anatumia vifaa vya zamani ambavyo ni shoka, patasi na msumeno.

Bw Juma anatafuta nafasi nzuri yenye kivuli chini cha miti ya mikoko ambayo imemea kando ya bahari na kuanza kuchonga gogo refu na nzito ambalo litakuwa uti wa mgongo wa jahazi lake, ambalo anatazamia kulikamilisha kwa muda wa miezi mitatu hivi.

Katika eneo la Pwani humu nchini, kuna baadhi ya maboti ya kitamaduni ambayo hadi wa leo bado yanatumika katika uvuvi na usafirishaji wa watu na mizigo.

Katika ufuo wa Ngare, kuna Mitumbwi kadhaa ambayo imeegeshwa kando ya bahari na ilitengenezwa kutoka kwa magogo ya miti mikubwa.

Bw Juma pia hutengeneza mitumbwi. Wavuvi wengi katika eneo hili huitumia katika shughuli zao za uvuvi kwa kuwa bei yake ni rahisi.

3.Mzee Ali Juma akiendelea kuchonga gogo litakalotumika kama uti wa mgongo wa jahazi ambalo anaendelea kulitengeneza. PICHA/ DIANA MUTHEU

Vyombo vingine vya aina hii ni ngalawa ambayo ni ndogo sana kiasi cha kwamba haiwezi kutumika katika bahari kuu.

Akiwa mzaliwa na mlelewa katika jamiii ya wavuvi, Bw Juma alianza uvuvi miaka 25 iliyopita.

“Nilianza uvuvi kitambo na baada ya kuvua kwa kipindi cha miaka 10, niliamua kuzingatia ufundi wa kutengeneza na kurekebisha maboti,” akasema Bw Juma ambaye ni baba wa watoto sita.

Bw Juma alisema kuwa alijifunza kutengeneza maboti kwa kutazama jinsi baba na babu yake walivyokuwa wakifanya. Alisema kuwa jahazi za kale zinazojulikana kama mashua hutengenezwa kwa muundo uliotokea nchi za Omani.

Ili kuunda jahazi hilo, Bw Juma anatumia mbao kutoka kwa mti wa mvinje (Casuarina). Mara nyingine huwa anatumia mbao ya mti wa mlozi (Almond).

Anasema jahazi lenyewe litatengenezwa kwa kuunganisha mbao ili kuunda sehemu ambayo watu wanaweza kuingia ndani na kuketi. Yeye huuzia wateja wake mashua hiyo kwa Sh300,000, na kufikia sasa ameuza majahazi saba.

Bw Juma anasema kuwa mtumbwi mdogo huuzwa kwa Sh12,000 na ule wa wastani kwa Sh20,000. Pia amekarabati mamia ya mitumbwi na kuuza minne. Mitumbwi huchukua muda mrefu kabla ziharibike.

Ili akarabati mitumbwi, Bw Juma huagiza Sh2,000 kutoka kwa wateja wake. Anasema ukarabati mwingi hufanywa wakati unaojulikana kama Kusi.

 “Babu yangu alitengeneza na kukarabati boti. Niliandamana naye kwenye safari zake za uvuvi na baadaye tukabakia ufuoni na kutengeneza boti. Vifaa vinavyotumiwa kujenga majahazi ni bora zaidi na chombo hicho cha majini kinaweza kukuhudumia kwa zaidi ya miaka 30,” akasema.

 Mita chache kutoka anapofanyia kazi, jahazi moja kwa jina MV Tetema limeegeshwa ufuoni. Lenyewe limepakwa rangi nyeusi na katikati limechorwa laini mbili kwa rangi nyekundu.

Mvuvi huyo anasema kuwa lina umri wa miaka 19 na amekuwa akilitumia katika uvuvi wake na pia kusafirisha watu na mizigo kutoka upande mmoja wa ufuo huo hadi mwingine-lilikuwa jahazi lake la kwanza kutengeneza.

Pia, ukubwa wa MV Tetema huweza kumfanya abiria kupunguza uwoga, ukilinganishwa na mitumbwi inayotumiwa na wavuvi katika eneo hilo la uvuvi.

“Maboti mengi huku yana uhusiano na mila na desturi ya Waswahili na watu wa eneo la Pwani,” akaongeza Bw Juma na kusema kuwa maboti ya kisasa ni ghali sana kwa mvuvi wa kawaida.

Alisema baadhi ya wateja wa kununua boti zake ni wavuvi ambao huagiza mitumbwi na mashua ndogo, huku jahazi zikinunuliwa na matajiri.

Jahazi la MV Tetema ambalo lina umri wa miaka 19 na lilitengenezwa na mzee Juma. PICHA/ DIANA MUTHEU

“Kuna wavuvi wengi eneo la Pwani ambao hutumia mashua na maboti katika shughuli zao za uvuvi,” akasema.

Kwa mazungumzo yake, Bw Juma alilinganisha umbo la vyombo hivyo vya majini na umbo la mifupa ya papa, ambapo gogo likifananishwa na uti wa mgongo na mbavu zikiwa mbao zilizounganishwa kutengeneza umbo la shimo ndogo.

Pia, mbao zaidi hupigiliwa ndani ya jahazi ili kumwezesha mvuvi au mtu yeyote kupata sehemu ya kuketi na hata kushikilia.

Bw Juma anasema kuwa kufikia sasa amewafunza vijana sita jinsi ya kukarabati maboti na pia wameweza kutengeneza mitumbwi na mashua ndogo.

Hata hivyo, mvuvi huyo alilalamika kuwa hakuna program katika kaunti ambayo inawapa nafasi wavuvi kama yeye wanaounda maboti kufikia soko kubwa.

“Idadi ya vijana ambao hawana ajira ni kubwa na kaunti inafaa kuangazia sekta kama hii kuwa kitega uchumi. Tuna bahari kubwa na kaunti yetu inafaa kutupiga jeki ili tuimarishe sekta ya uvuvi,” akasema.

Aliongeza kuwa ufundi wa kutengeneza maboti umemfunza kuwa mvumilivu na mkakamavu, na pia anapata riziki kupitia kazi hiyo.

You can share this post!

Miili ya wawili yaopolewa kisimani shughuli ya kutafuta wa...

Serikali yahakikishia wawekezaji sekta ya utalii kwamba...