Habari Mseto

COVID-19: Wanawake wapiku wanaume

September 8th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

KWA mara ya kwanza Jumanne, idadi ya wanawake walioambukizwa Covid-19 imezidi ile ya wanaume tangu kisa cha kwanza cha ugonjwa huo kithibitishwe nchini.

Kulingana na takwimu iliyotolewa na Wizara ya Afya, miongoni mwa watu 151 waliopatikana na virusi vya corona 77 walikuwa wa jinsia ya kike.

Wagonjwa hao wapya walipatikana baada ya sampuli 2,552 kupimwa.

Tangu kisa cha kwanza cha Covid-19 kisajiliwe nchini Kenya mnamo Machi 13, 2020, idadi na wanaume wanaombukiza ndani ya muda wa saa 24 imekuwa juu ikilinganishwa na ile ya wanawake.

Hali hiyo imeibua maswali mengi miongoni mwa wanasayansi na wataalamu wa kiafya.

Mnamo Jumanne Waziri Msaidizi wa Afya Rashid Aman alisema kuwa baada ya maambukizi hayo 151 kunakiliwa, idadi jumla ya maambukizi imefika 35,356 kufikia Jumanne.

Jumla ya sampuli 479,697 zimepimwa tangu mwezi Machi 2020.

Wakati huo huo, Dkt Aman alionya Wakenya dhidi ya kufasiri kupungua kwa idadi ya maambukizi kuashiria kupungua kwa makali ya janga hilo nchini, akisema kuwa idadi ya maambukizi imepanda katika baadhi ya kaunti.

“Idadi ya maambukizi inapanda katika baadhi ya kaunti kama vile Kitui. Hii ndio maana tunapaswa kuwa waangalifu tunapochambua idadi ya maambukizi,” akasema.

Dkt Aman alisema kaunti zingine kama vile Meru, Kajiado, Machakos, Busia na Nyeria pia zimeshuhudia ongezeko la visa vya maambukizi ya Covid-19.