Habari

Mishi Mboko ataka wanasiasa waonyeshe ukomavu hata wanapotofautiana

September 9th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MISHI GONGO

MBUNGE wa Likoni Bi Mishi Mboko amewataka wanasiasa wakome kutaja baadhi ya sehemu za mwili, hasa wa mwanamke, wanapochambana hadharani akisema kufanya hivyo ni kuwadhalilisha wanawake.

Alisema hayo nje ya bunge la Kaunti ya Mombasa ambako alikuwa ameandamana na wanawake kutoka maeneo mbali mbali ya mji huo.

Bi Mboko aliwasuta wabunge Johanna Ng’eno (Emurua Dikirr) na Oscar Sudi (Kapseret) kwa kile alikitaja ni kutoa matamshi yanayomkosea heshima Rais Uhuru Kenyatta na familia yake.

“Matiti ndiyo yaliyowalea, ni ukosefu wa adabu kusimama hadharani na kutaja viungo vya wanawake hasa katika kauli zinazoonyesha wazi ni kuchambana,” akasema Bi Mboko.

Bi Mboko hasa aliwataka wabunge hao wajifunze ustaarabu hata katika kuonyesha kukasirishwa kwao.

Aliongezea kuwa Handisheki kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga imesaidia kudumisha amani nchini hivyo inafaa kuungwa mkono.

Alielezea imani yake kuwa kiongozi wa nchi ataendeleza vita dhidi ya ufisadi na kuwa wote wanaohusika watachukuliwa hatua.

Aliwaambia mahasimu wa Rais kuwa matusi yao hayatamtikisa katika kutekeleza kazi yake.

“Uhuru yuko hapa na ataendelea kuwa. Kama mnataka siasa subirini mwaka 2022. Acheni kuingiza matusi katika kampeni mnazopiga, huo ni utovu wa nidhamu na mnapotosha vijana,” akasema Bi Mboko.