Habari

Maseneta Kwamboka, Mary Seneta wapatikana na hatia

September 9th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

MASENETA maalum Beatrice Kwamboka na Mary Seneta wametakiwa kuwaomba msamaha maseneta wenzao kufuatia kisa ambapo walipigana hadharani katika kikao cha Kamati ya Seneti kuhusu Afya miezi miwili iliyopita.

Watahitajika kuomba msamaha mbele ya kikao cha maseneta wote kabla ya kuruhusiwa kushiriki katika shughuli zozote za bunge hilo au kamati zake.

Hii ni baada ya Kamati ya Seneti kuhusu Mamlaka na Hadhi ya Seneti kuwapata na hatia ya kushusha hadhi na heshima ya bunge hilo kutokana na kitendo hicha cha aibu.

Maseneta hao wawili walirushiana makonde na cheche za matusi wakati wa uchaguzi wa Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Afya mnamo Julai 6, 2020.

Bi Kwamba na Bi Seneta walitofautiana kuhusu azma ya Seneta wa Narok Ledama Ole Kina ya kuchaguliwa kwa wadhifa huo bila kupinga.

“Kamati ya Mamlaka na Hadhi ya Seneti inapendekeza kwamba kulingana na sehemu ya 17 (3) (b) ya Sheria ya Mamlaka na Hadhi ya Bunge, Seneta Beatrice Kwamboka na Seneta Mary Seneta wakaripiwe kwa kukiuka hadhi na heshima ya bunge hili. Wanaamriwa kuomba msamaha kwa kikao kizima cha Seneti kwa kusoma taarifa ya msamaha huo baada ya kuidhinishwa na Spika,” ripoti ya kamati hiyo ikasema.

Kamati hiyo inaongozwa na Spika wa Seneti Kenneth Lusaka.

Kamati hiyo inaongeza kuwa iliwapata maseneta hao wawili na makosa “na kinyume na hitaji la Sura ya Sita ya Katiba na Sheria za Seneti.

Maseneta Kwamboka na Seneta walifika mbele ya Kamati hiyo ambapo walijitetea.

Akijitetea Bi Kwamboka ambaye ni Seneta Maalum wa ODM alidai kuwa alilazimika kumkabili Bi Seneta alipomtusi. Naye Bi Seneta alieleza kusikitishwa na tukio hilo akisema wamesuluhisha tofauti zao na wanaendelea kushirikiana bila tatizo lolote.

Kisa hicho pia kiliripotiwa kwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) ilisema kitendo hicho kinaenda kinyume cha hitaji la maadili kwa Maafisa wa Serikali “kulingana na Sura ya Sita ya Katiba na Sheria kuhusu Uongozi na Maadili kwa Maafisa wa Umma, 2012.”