Giroud asaidia Ufaransa kupiga Croatia 4-2 na kunusia rekodi ya Thierry Henry
Na MASHIRIKA
MSHAMBULIAJI wa Chelsea, Olivier Giroud alifunga bao lake la 40 kimataifa na kusaidia Ufaransa kuwapepeta Croatia 4-2 katika gozi la UEFA Nations League mnamo Septemba 8, 2020.
Mechi hiyo ilirejesha kumbukumbu ya fainali ya Kombe la Dunia mnamo 2018 nchini Urusi ambapo Ufaransa walizamisha pia Croatia idadi sawa na hiyo ya mabao na kutwaa ubingwa.
Katika mchuano huo ambao ulikuwa wa 99 kwa Giroud kuchezea Ufaransa, nyota huyo wa zamani wa Arsenal alitokea benchi katika kipindi cha kwanza na kufunga bao katika dakika ya 77 kupitia penalti.
Ufanisi huo sasa unamsaza akihitaji bao moja pekee ili kufikia rekodi ya nguli wa soka Michel Platini aliyefungia timu ya taifa ya Ufaransa jumla ya mabao 39 katika kabumbu ya kimataifa.
Aliyekuwa gwiji wa soka kambini mwa Arsenal, Thierry Henry, ndiye mshikilizi wa rekodi ya ufungaji bora katika timu ya taifa ya Ufaransa kwa mabao 51.
Beki wa zamani wa Liverpool, Dejan Lovren aliwaweka Croatia kifua mbele kunako dakika ya 16 kabla ya fowadi Antoine Griezmann wa Barcelona kusawazisha mambo katika dakika ya 43.
Ingwa Ufaransa walifunga bao la pili mwishoni mwa kipindi cha kwanza kupitia kwa Dominik Livakovic aliyejifunga, Croatia walirejeshwa mchezoni na Josip Brekalo katika dakika ya 55.
Difenda Dayot Upamecano anayehusishwa na uwezekano wa kutua Arsenal au Manchester United kutoka RB Leipzig ya Ujerumani, alifungia Ufaransa bao la tatu katika dakika ya 65 kabla ya Giroud kufunga kazi dakika 12 baadaye.
Ushindi wa Ufaransa unawadumisha kileleni mwa Kundi 3 kwenye kivumbi cha Nations League sawa na mabingwa watetezi Ureno watakaokuwa wageni wao jijini Paris Oktoba.
Eduardo Camavinga aliyetokea benchi katika dakika ya 63 akiwa na umri wa miaka 17 mna siku 303 aliweka historia ya kuwa mchezaji mchanga zaidi kuwahi kuchezea timu ya taifa ya Ufaransa baada ya Maurice Gastiger mnamo Februari 1914.
Kwingineko, Ubelgiji walitoka nyuma na kufungiwa mabao mawili ya haraka na fowadi Michy Batshuayi katika ushindi wa 5-1 waliousajili dhidi ya Iceland. Batshuayi anahusishwa na uwezekano mkubwa wa kurejea kambini mwa Crystal Palace katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).