Habari

CoG yashutumiwa kwa kuzima matangazo ya biashara na NMG

September 9th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

BARAZA la Vyombo vya Habari Nchini (MCK) limelikashifu baraza la magavana (CoG) kwa kuagiza serikali za kaunti kuzima matangazo yote ya kibiashara kwa Shirika la Habari la Nation (NMG) baada ya kuchapisha habari waliodai inawasawiri baadhi ya magavana kama mafisadi.

Amri hiyo ilitolewa kwa magavana wote 47 kwenye taarifa iliyotolewa na mwenyekiti wa CoG Wycliff Ambetsa Oparanya Jumanne, Septemba 8, 2020.

Lakini kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Jumatano, Septemba 9, 2020, MCK imesema hatua hiyo ya CoG ni yenye nia mbaya na ni tisho kwa uhuru wa vyombo vya habari.

“Baraza la Vyombo Habari Nchini linalaani taarifa iliyotolewa na Baraza la Magava Jumanne, Septemba 8, 2020, kuhusu namna shirika la habari la Nation liliripoti habari kuhusu madai ya magavana kuhusishwa na ufisadi,” baraza hilo likasema.

MCK ilisema inaheshimu haki ya CoG ya kulalamika kuhusu habari zilizochapishwa katika vyombo vya habari. Lakini ikasema magavana wanapaswa kuwasilisha malalamishi yao kwa asasi hiyo na hawafai kuchukua hatua yoyote inayoonekana ya kuadhibu shirika lolote la habari kwa njia yoyote.

“Malalamishi yoyote dhidi ya mwanahabari au shirika la habari ni vizuri yakiwasilishwa kwa tume ya kushughulikia malalamishi kuhusu sekta ya habari, asasi inayosimamiwa na MCK. Malalamishi hayo yatasikizwa na hatua mwafaka kuchukuliwa. Huu ndio utaratibu unaotambuliwa na sheria zinazosimamia sekta ya habari nchini na unapaswa kufuatwa na umma,” taarifa hiyo ikasema.

Baraza hilo lilisema endapo mwanahabari yeyote atashambuliwa akiwa kazini, kutokana na tangazo la CoG, litaelekeza lawama kwa magavana hao wakiongozwa na mwenyekiti wa baraza hilo Bw Oparanya.

Wamiliki wa vyombo vya habari kupitia mwenyekiti wa chama chao (MOA) Wachira Waruru pia wameshutumu CoG kwa kusitisha biashara na NMG kwa kuandika habari zinazowahusisha magavana na ufisadi.

Kwenye taarifa Bw Waruru amesema endapo magavana wana malalamishi yoyote kuhusu habari zilizochipishwa katika vyombo vya habari wanapaswa kuyawasilisha kwa baraza la vyombo vya habari (MCK).

“Hatua ya kusitisha biashara na NMG ni sawa na kuhujumu uhuru wa vyombo vya habari ambao unalindwa na Katiba ya nchi,” akasema Bw Waruru ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Habari la Royal Media Services.

Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen pia alikashifu hatua hatua hiyo ya baraza la magavana akisema “ni kinyume cha sheria”.

“Stori kuhusu gavana sio kuhusu kaunti. Matangazo ya kibiashara hayapaswi kutolewa kwa mapenzi ya magavana. Hii ni kinyume cha sheria za ununuzi wa bidhaa na huduma za umma. Magavana ambao wanatajwa katika sakata za ufisadi wabebe msalaba wao na wakome kuingiza kaunti zao katika maovu hayo,” Bw Murkomen akasema kupitia mtandao wa Twitter.