• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
TAHARIRI: Serikali itoe kauli kuhusu masharti

TAHARIRI: Serikali itoe kauli kuhusu masharti

Na MHARIRI

KWA karibu wiki mbili sasa tangu idadi ya maambukizi ya virusi vya corona inayotangazwa kila siku ilipoanza kupungua, serikali imekuwa ikisisitiza Wakenya waendelee kufuata kanuni za kuepusha ueneaji wa maambukizi.

Hii ni kutokana na kuwa, kwa kuzingatia matukio katika mataifa mengine ya nje, kungali kuna uwezekano wa maambukizi kuanza kuongezeka tena.

Wakati huo huo, ushauri huo umesababishwa na jinsi takwimu zinavyoonyesha maambukizi yanaanza kuwa mengi katika kaunti kadha ambazo hazikuwa na wagonjwa wengi awali kama vile Kitui, huku idadi ikipungua katika kaunti ambazo zilikuwa na maambukizi mengi kama vile Nairobi.

Hitaji la watu kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo wa Covid-19 ni muhimu kwa vile hakuna aliye na uhakika kufikia sasa kuhusu hali ya baadaye.

Hata hivyo, haitakuwa rahisi kwa serikali kuwashawishi wananchi waendelee kufuata masharti makali yaliyopo kwani viongozi wangali katika mstari wa mbele kuvunja masharti hayo.

Tangu janga la corona lilipothibitishwa kuingia nchini mnamo Machi, si siri kwamba kumekuwa na ubaguzi katika utekelezaji wa masharti yaliyotangazwa.

Wananchi walijionea jinsi viongozi wengi wa kisiasa walivyoachwa kuendelea na shughuli zao za kawaida, ilhali akina yakhe walitaabika mikononi mwa polisi hadi wengine wakaripotiwa kuuawa kwa misingi duni kama vile kukosa kuvaa barakoa.

Wakati huu ambapo idadi ya maambukizi imeanza kupungua, itabidi serikali itafute mbinu nyingine za kushawishi wananchi kuhusu hitaji la kuendelea kufuata masharti yaliyowekwa au masharti mapya ambayo huenda yakatangazwa hivi karibuni.

Hii ni kutokana na kuwa, mikutano ya kisiasa inaendelea kwa wingi katika pembe tofauti za nchi ilhali raia wa kawaida anakatazwa kuandaa mikutano ya halaiki.

Hivi majuzi, mawaziri kadha pia walionekana kwenye video wakijiburudisha kwa nyama bila kujali kanuni za kutotagusana ilhali mlala hoi anashauriwa kuepuka mienendo hiyo hiyo.

Ni matukio aina hii ambayo yanafanya wananchi kukosa imani kwa yale ambayo wanaagizwa kufanya na serikali.

Hivi sasa, wengi wameanza kupuuza karibu kanuni zote wazi bila kujali kama kungali kuna hatari ya maambukizi huko nje wanapokutana na watu.

You can share this post!

AWINO: Konokono Mwea wasipuuzwe kama gugumaji Victoria

NGILA: Afrika yote ifuate Somalia kwa Intaneti ya bei nafuu