Miradi ya vivukio Thika Superhighway yasababisha misongamano
Na SAMMY WAWERU
KWA muda wa wiki kadhaa msongamano wa magari umekuwa ukishuhudiwa Thika Superhighway, kufuatia utengenezaji wa madaraja na vivukio vya barabarani.
Madaraja hayo yanayotengenezwa eneo la Garden City – Homeland na Survey, shughuli hiyo inaendeshwa na Halmashauri ya Barabara Kuu Nchini; KenHA.
Ujenzi huo umeendelea kusababisha msongamano wa magari, ambao wakati mwingine huanza eneo la Ksarani.
“Tunafahamisha umma ujenzi wa daraja Garden City unaendelea, wenye magari watumie njia mbadala kufika jijini Nairobi au kuelekea Ruiru na maeneo mengine yanayotumia Thika Road,” KeNHA ikaarifu kwenye mojawapo ya notisi.
Maeneo yanayojengwa daraja yanasemekana kuchangia msongamano wa magari Thika Road, kufuatia watu wanaovuka kwa miguu sehemu zilizotengenewa shughuli hiyo.
Maafa pia yamekuwa yakishuhudiwa, kutokana na maderevu tepetevu wasioheshimu umma unaovuka.
Madaraja hayo yakikamilika, yatasaidia kupunguza ajali za wanaogongwa na gari wakivuka pamoja na kupunguza msongamano.