• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 12:26 PM
NAIBU GAVANA NAIROBI: Jina la Miguna lawasilishwa kwa spika Elachi

NAIBU GAVANA NAIROBI: Jina la Miguna lawasilishwa kwa spika Elachi

Na CHARLES WASONGA

SPIKA wa Bunge la Kaunti ya Nairobi Beatrice Elachi amethibitisha kwamba Gavana wa Nairobi Mike Sonko amemteua mwanasheria mbishi Miguna Miguna kuwa naibu wake.

“Gavana ametupea jina la mtu aliyempendekeza kwa wadhifa wa naibu gavana. Tutafuata sheria. Katiba inasema wazi kuwa naibu gavana anapaswa kuwa Mkenya,” akasema Bi Elachi

“Ningependa kumshauri Miguna kusuluhisha masuala yake na Serikali ya Kenya kwanza kwani yeye ni Raia wa Canada. Utaratibu huo unaweza kuchukua muda wa miezi mitatu au minne,” akaongeza Bi Elachi alipokuwa akihojiwa kwenye kituo cha redio cha Hot 96 FM.

Mnamo Jumatano jioni wakili wa Dkt Miguna, Cliff Ombeta alithibitisha kuwa Bw Sonko amemteua mwanasiasa huyo mbishani kuwa Naibu wake.

Hatua hiyo iliwashangaza wengi ikizingatiwa kuwa Miguma ni mmoja wa wakosoaji wakubwa wa Gavana Sonko.

Mkurugenzi wa Mawasiliana katika Kaunti ya Nairobi Elkana Jacob alisambaza barua ya uteuzi wa Miguna katika ukurasa wake wa Facebook lakini wengi walishuku uhalali wake.

Maafisa wakuu katika makao makuu ya kaunti ya Nairobi, City Hall, hawakuwa tayari kuthibitisha habari hizo.

Hata hivyo, kufikia sasa, Dkt Miguna hajakubali wala kukataa uteuzi.

Gavana Sonko amekuwa akishinikizwa kumteua naibu wake baada ya Polycarp Igathe kujiuzulu mapema mwaka huu akidai kunyimwa “uhuru wa kutekeleza majukumu yangu kwa manufaa ya wakazi wa Nairobi.”

Bw Ombeta alisema jina la Miguna limewasiliwashwa kwa Spika wa Bunge la Nairobi kwa uchunguzi na madiwani.

“Ndio ni kweli, na naelekea City Hall asubuhi ya kuchukua barua ya uteuzi wa Miguna,” akasema Bw Ombeta.

Bw Miguna, ambaye yuko nchini Canada baada ya kufurushwa kutoka nchini, aliwania ugavana wa Nairobi katika uchaguzi mkuu wa 2017.

Mwanasiasa huyo alikuwa ametangaza kuwa angerejea nchini Jumatano lakini akaahirisha safari hiyo. Hii ni baada ya Idara ya Uhamiaji kukataa kushikilia kuwa sharti ajaze fomu za kumrejeshea uraia wa Kenya kabla ya kupewa paspoti halali.

Mahakama Kuu ilikuwa imeiamuru Idara ya Uhamiaji kumsaidia Dkt Miguna kurejea humu nchini baada ya kufutilia mbali amri ya Waziri wa Masuala ya Ndani Fred Matiang’i ya kumtaja kama mhamiaji asiyekubaliwa nchini.

“Nilikuwa nikitarajia kufika nyumbani kulingana na mpangilio wangu. Lakini nikaahirisha safari hiyo hadi wakati mwingine,” akasema Bw Miguna.

Utata unaozingira suala la uraia wa Dkt Miguna bado unaendelea huku wakili huyo akisubiriwa kufuata masharti ya serikali.

You can share this post!

Mfumo mpya wa Safaricom kusaidia kuzima wizi

Hauwezi kumlazimishia Miguna jambo – Ombeta

adminleo