• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 6:27 PM
LISHE: Jinsi ya kutayarisha achari ya mbirimbi

LISHE: Jinsi ya kutayarisha achari ya mbirimbi

Na MISHI GONGO

ACHARI ya mbirimbi ni pilipili iliyotengezwa kwa mbirimbi. Hutumika kuongezea chakula ladha.

Watu wa Pwani hasa Waswahili hupenda sana kula vyakula vyao wakiongezea pilipili ya kupika.

Pia unaweza kutengeza achari ya ndimu, maembe, kamba na chicha za nazi.

Vitu vinavyohitajika

  • mbirimbi kiasi unachotaka
  • pilipili nyekundu vipande 5
  • nyanya 2
  • kitunguu maji kikubwa 1
  • kitunguu thomo tembe 4
  • mafuta ya uto kikombe 1/2
  • manjano kijiko 1
  • chumvi vijiko vya chai 2

Jinsi ya kutayarisha

Loweka mbirimbi katika maji moto kwa dakika 10 kisha zitoe kwa kutumia kisu. Zipasue uzitoe mbegu kisha weka pembeni.

Chukua pilipili, vitunguu na nyanya kisha usage pamoja hadi kuvurujika.

 

Bandika sufuria motoni kisha tia mafuta ya uto yakishapata mimina rojo ya nyanya na vitunguu ulivyosaga. Acha rojo itokote kwa dakika tano kisha ongeza mbirimbi zako kavu.

Acha zitokote kwa muda wa dakika tano kisha epua na uweke pembeni ukisubiri vipoe.

Zikashapoa, weka katika chombo cha mfuniko na unaweza kuanza kutumia.

Unaweza kula achari hiyo kwa wali, pilau, matoke na kadhalika.

Mbirimbi inasemekana kuwa na manufaa mengi mwilini kwa mfano hupunguza joto mwilini, kupunguza cholesterol na kutibu chunisi na kuondoa madoadoa.

You can share this post!

Serikali yasaka Sh100 bilioni kufufua biashara

TAHARIRI: Uwakilishi wa jiji katika baraza la mawaziri wafaa