• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 5:55 AM
Wanawake waliopigania uhuru wakati wa Maumau wawataka wanasiasa waonyeshe ukomavu

Wanawake waliopigania uhuru wakati wa Maumau wawataka wanasiasa waonyeshe ukomavu

Na LAWRENCE ONGARO

WANAWAKE waliopigania Uhuru wakati wa Maumau wapatao 40 kutoka Kaunti ya Kiambu, wamejitokeza wazi wakiwataka wanasiasa waache kutoa matamshi yanayoonekana kuikosea heshima familia ya Rais Uhuru Kenyatta.

Wanawake hao waliwashauri viongozi wawili kutoka Bonde la Ufa; Johana Ng’eno na Oscar Sudi wawe na heshima kwa Rais Uhuru Kenyatta, hasa asasi ya urais anayoshikilia.

Pia alikuwepo aliyekuwa mwakilishi wa wanawake Kiambu katika Bunge la Kitaifa, Bi Anne Nyokabi, aliyesema heshima ni kitu cha muhimu katika maisha ya binadamu na kwa hivyo viongozi wanastahili kuelewa maana yake.

Wanawake hao walioonekana wenye hasira walikongamana katika uwanja wa michezo wa Ndumberi, Kaunti ya Kiambu na kusema Wakenya wanahitaji amani.

“Tukikumbuka jinsi wakoloni walivyowatesa wanawake kwa kuwadhulumu tunasikia uchungu mwingi sana. Kwa hivyo watu wanaotaka kuleta taharuki wasikubaliwe,” alisema mmoja wa wanawake hao wakongwe.

Walisema waume zao waliteswa vibaya huku wakitiwa kizuizini na kukoseshwa amani.

Kwa hivyo wale wanaotaka kuleta machafuko wakome kabisa, ndiyo ilikuwa kauli yao.

Walisema Mama Ngina Kenyatta, alipitia magumu wakati mumewe Rais wa Kwanza wa Kenya huru Mzee Jomo Kenyatta Kenyatta, alipokuwa kizuizini Kapenguria na kwa hivyo yeyote anayejaribu kuikejeli familia hiyo anafaa kufikiria mara mbili kabla ya kutoa matamshi hayo.

Walisema yeyote aliyeshiba aache kuvuruga wengine lakini badala yake ahubiri amani kwani “nchi hii ni ya amani.”

“Wale wanaoendelea kumsuta Rais Uhuru Kenyatta wakome kwani Rais anataka kuona Kenya ikiwa na amani na kila mmoja anajisikia akiwa salama,” alisema Bi Nyokabi.

Alisema wale wanaoteta wamwache kiongozi wa nchi akamilishe ajenda yake ya kutumikia wananchi huku akijiandaa kustaafu kwa amani.

“Kila Mkenya anastahili kupewa nafasi kuendesha mambo yake kwa amani bila kutatizwa. Wakenya ni watu wenye bidii na ni vyema kupewa nafasi kuendesha shughuli zao kwa amani,” alisema Bi Nyokabi.

You can share this post!

JAMVI: Azma ya urais ya Wa iria kuchemsha mikimbio ya...

Ruto amzidi Uhuru, Raila