• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
BBI si chombo cha kujitakia mamlaka – Raila

BBI si chombo cha kujitakia mamlaka – Raila

Na MISHI GONGO

KIONGOZI wa ODM, Raila Odinga amesema kuwa Mpango wa Maridhiano BBI haulengi kuwatengezea nafasi viongozi watakaoangushwa katika uchaguzi mkuu.

Akizungumza hapo Jumamosi katika mkutano na wawakilishi wa vikundi mbalimbali katika ukumbi wa Wildwaters mjini Mombasa, mwanasiasa huyo alisema Mpango wa Maridhiano utaangazia masuala kama wanawake kupewa nafasi zaidi, pamoja na kuongeza mgao wa kaunti hadi asilimia 35 kutoka kwa asilimia 10 inayopendekezwa.

Bw Odinga alisema kuwa Mpango huo pia haulengi kubadilisha Katiba bali kuiboresha kwa maslahi ya Wakenya.

“Mpango wa Maridhiano haupangi kuwapa watu pesa wala nafasi kama vile inavyosemekana. Hatutaki Kenya ya kuwapa watu samaki aliyetayarishwa bali tunataka kuwafundisha watu kuvua,” akasema Bw Odinga.

Katika ziara hiyo Bw Odinga aliandamana na Gavana Hassan Joho (Mombasa), Mbunge wa Kike wa kaunti hiyo, Bi Asha Hussein, wabunge Abdulswamad Sheriff Nassir (Mvita), Mishi Mboko (Likoni), Badi Twalib (Jomvu) Omar Mwinyi (Changamwe), Seneta wa Kaunti ya Kwale Issa Boy, wawakilishi wa jamii za Pwani na wafuasi wengine wa ODM mjini Mombasa.

Gavana Joho alisema kuna haja kwa wakazi wa Pwani kufanya kazi pamoja ili kufikia malengo ya kuwa na kiongozi wa kitaifa.

“Tuache hizi porojo za chini kwa chini. Mmoja wetu akisimama tumuunge mkono na si kumvunja moyo na kusema kuwa hawezi,” akasema Bw Joho.

Wawakilishi waliyohudhuria mkutano huo walisisitiza masuala ya ardhi, uchumi wa baharini (blue economy) na bandari kuongezewa katika mpango huo ili kuwanufaisha Wapwani ambao wanadai wametengwa kwa muda mrefu.

  • Tags

You can share this post!

Maswali mengi polisi 300 wakijaribu kukamata Sudi nyumbani...

Walimu walalamikia mwongozo mpya wa kuwapandisha vyeo