TAHARIRI: Polisi wazuie visa vya uhuni wa vijana
Na MHARIRI
VISA vya wiki jana vilivyohusisha vijana kushambulia watu kwa mirengo ya kisiasa ni ishara mbaya kwa nchi yetu, karibu miaka miwili kabla ya Uchaguzi Mkuu.
Katika juhudi za kujiweka kaatika nafasi nzuri ya kuonekana na wapiga kura, wanasiasa mbalimbali wameanza kutambua udhaifu mkubwa uliopo miongoni mwa vijana.
Wanatambua kwamba ukosefu wa ajira unaweza kuwafanya vijana kutenda lolote kwa hela kidogo au ahadi tu kuwa mwisho wa siku watapata kitu.
Makabiliano mabaya yaliyotokea kati ya wandani wa Naibu Rais William Ruto na wale wanaounga mkono handisheki ya Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga katika Kaunti ya Kisii, si dalili nzuri.
Vijana wengine walikusanyika na kuandamana na mbunge wa Emurua Dikirr, Johanna Ng’ eno alipoachiliwa kutoka kituo cha polisi. Mbunge huyo alikuwa amezuiliwa kwa madai ya uchochezi na baadaye akafikishwa katika mahakama mjini Nakuru.
Hali sawa na hiyo ilishuhudiwa katika Kaunti ya Meru ambako vijana walimshambulia mbunge wao, huku vijana wengine wakijaribu kukabiliana na polisi ili kuwazuia wasimkamate Mbunge wa Kapseret, Oscar Sudi.
Miaka ya 2007 na 2017 kulipozuka fujo baada ya Uchaguzi Mkuu, ni kina mama na watoto walioathiriwa kwa kukosa makao au hata kuuawa.
Siku zote ghasia zinapotokea, huwa wanasiasa hawaathiriki isipokuwa watu ambao kamwe hawajihusishi na uhuni huo.
Wahuni huchukua fursa kubaka watu, kuwaua wengine kwa mishale au mapanga huku polisi nao wakiua kwa risasi.
Japokuwa Wakenya wanakumbuka vyema jinsi fujo kama hizi zilivyokaribia kuitumbukiza nchi katika maangamizi, inaonekana wazi kuwa vijana hawajajifunza chochote.
Viongozi wa makanisa na wadau wengine waliojitokeza kukemea vurugu na matamshi ya chuki, wanapaswa kuchukua hatua zaidi ili kuiepusha nchi na janga linaloweza kuzuiwa.
Huu ni muda mzuri kwa polisi kuonyesha kwamba wanaijali nchi yao, kwa kuwachukulia hatua wahusika wote, bila ya kujali nyadhifa zao serikalini au katika jamii.
Kwa kuwaruhusu watu watusiane au kuandamana barabarani wakitetea wanasiasa, polisi wanapalilia mbegu ya uasi, ambayo itakuwa vigumu kung’oa mizizi yake mambo yakiwa mabaya.