Kenya yakataa mkataba wa Uchina kulinda biashara zake
Na BERNARDINE MUTANU
Kenya imekataa kutia sahihi mkataba wa kibiashara ambao serikali ya China imekuwa ikisukuma mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuidhinisha tangu 2016.
Ripoti hii ni kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi na Biashara Bw Chris Kiptoo.
Jumatatu Mei 14, Bw Kiptoo alisema uamuzi huo ulitokana na haja ya kuzilinda kampuni za Kenya.
Hii ni kutokana na kuwa Kenya ikikubali mkataba huo huenda ukaathiri kampuni za humu nchini ambazo ni changa, kwa sababu ya bidhaa za China za bei ya chini.
Huenda hatua ya Kenya ikazua mgogoro wa kidiplomasia kati yake na China. Kwa sasa, biashara kati ya EAC na China inapendelea zaidi taifa hilo.
Kwa sasa miongoni mwa bidhaa zinazonunuliwa nje ya nchi, asilimia 25 hutoka China.
Hivyo, kuidhinishwa kwa Eneo la Biashara Huru (FTA) ni kumaanisha kuwa bidhaa kutoka China zitaongezeka nchini zaidi, na kulemaza bidhaa zilizotengenezewa humu nchini.
Hata hivyo, bidhaa ambazo Kenya huuza nchini China ni za chini zaidi (asilimia mbili) ya bidhaa zote zinazouzwa kutoka Kenya nje ya nchi.