ODM kutumia kura ya maoni kupata mgombea ubunge
Na FADHILI FREDRICK
CHAMA cha Orange Democratic Movement (ODM) kitatumia kura za maoni kumchagua mgombea atakayekiwakilisha katika kinyang’anyiro cha uchaguzi mdogo wa eneobunge la Msambweni, kaunti ya Kwale.
Kinara wa chama hicho, Bw Raila Odinga alisema kura hizo za maoni zitaleta usawa katika mchakato wa uteuzi wa mgombea, atakayemenyana na wengine katika uchaguzi huo mdogo.
Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) bado haijatangaza siku ya uchaguzi kutokana na janga la corona.Kiti hicho kiliachwa wazi baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge wa Msambweni , Suleiman Dori Machi 9, mwaka huu.
Akihutubia wanachama na viongozi wa chama hicho katika hoteli ya Jacaranda Diani, Bw Odinga alisema kura ya maoni itakayofanywa na wataalamu ndiyo itakayokuwa njia nzuri ya kupata mgombeaji.
“Hakuna mtu atakayechaguliwa na chama. Tunataka uwazi na haki ili tuweze kuwathibitishia wapinzani wetu kwamba Msambweni kweli ni ngome ya ODM,’ akasema.
Chama hicho kinataka kuharakisha mchakato wa uteuzi, ili kuwa na muda wa kutosha wa kampeni. Akiandamana na Gavana wa Mombasa Hassan Joho, Mwakilishi wa Wanawake Kwale Bi Zuleikha Juma na Seneta wa Kwale Bw Issa Juma Boy, aliwahimiza wagombea pia kufanya mazungumzo na kukubaliana kati yao juu ya nani atakayeachia kiti hicho mwengine kabla kura ya maoni kufanywa.
Tayari wagombea wanne akiwemo alikuwa mwakilishi wadi Bongwe/Gombato Idd Boga, Mariam Akinyi, Nicholas Zani ambaye ni naibu mwenyekiti wa chama tawi la Kwale na Feisal Bader wamejitokeza kugombea kiti hicho kupitia chama cha ODM.
Bader ni jamaa wa karibu wa Dori ambaye anataka kutekeleza urithi wake.Hata hivyo Bw Raila alisema iwapo njia hizo mbili zitashindwa, chama basi kitaenda kwa uteuzi kupitia kura za mchujo.
Aidha aliwahimiza wale watakaoshindwa katika mchujo huo kuunga mkono mshindi, akisema hatua hiyo itaimarisha chama na kufanikiwa kuchukua kiti hicho.
‘Ningesisitiza kwamba wacha tuungane pamoja chini ya makubaliano moja kunyakua kiti cha ubunge hata ikiwa hautapitia uteuzi,’ alisema.
Joho aliwatahadharisha wanachama kutogawanywa akisema mgawanyiko utachangia katika kupoteza nafasi ya ubunge eneo hilo.Vile Bw Joho alisema michujo ya chama ya awali ndio ilichangia chama hicho kupoteza viti vingi vya uchaguzi na vyama pinzani.
‘Lazima tujirekebishe na kuwa na uwazi katika kutafuta mgombea wa chama. Kufanya kosa sio kosa lakini kurudia kosa ndio makosa. Tumejua ni wapi tulikosea katika michujo na ndio chama hakitakuwa na uteuzi wa moja kwa moja kwa wagombeaji,’ akasema.
Bw Joho aliwahimiza wagombea kuunga mkono mgombea atakayefaulu kuwakilisha chama na kuonyesha mshikamano.? ‘Msichukuliane kama maadui kwa sababu ninyi ni wapinzani, bali tunastahili kuwa pamoja hadi tuchukue ushindi,’ akasema Joho.
Ziara hiyo wa Kinara wa chama ilelenga kuwatambua wagombeaji wa uchaguzi mdogo huo na kuwaunganisha wanachama ikiwa na matayarisho ya uchaguzi huo.