• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 1:51 PM
Mashirika yatetea wauguao Ukimwi

Mashirika yatetea wauguao Ukimwi

NA DIANA MUTHEU

MASHIRIKA ya kibinafsi yanayowashughulikia wagonjwa wa virusi vya ukimwi yanaitaka serikali ya kaunti ya Mombasa iwape waathiriwa msaada wa vyakula na pesa za kuanzisha biashara.

Wakizungumza na Taifa Leo walipokuwa wanatoa msaada wa vyakula kwa vijana 100 ambao wana virusi hivyo katika kliniki ya Mvita Sub-County, maafisa kutoka shirika la Dreams Achievers Youth (DAYO) na Aids Healthcare (AHF) walisema watu walioambukizwa virusi vya ukimwi wanafaa kupata lishe bora, kwa kuwa wako katika hatari kubwa iwapo watapata maradhi ya Covid-19.

Afisa wa miradi wa DAYO, Enos Opiyo alisema mpango huo utawafikia vijana 300 katika kaunti ya Mombasa ili kuwaepusha na matatizo kadhaa ya kiafya wanapokosa kupata lishe bora.

“Wagonjwa wa ukimwi ni moja ya makundi yaliotajwa kuwa katika hatari ya kuambukizwa virusi vya corona, lakini wakipata misaada kama hii, wataweza kuwa na kinga ya juu mwilini,” akasema Bw Opiyo.

Afisa wa kliniki hiyo, Dkt Khadija Awadh alisema kuwa bidhaa hizo zitasambazwa katika hospitali zote za maeneo bunge, ili wagonjwa hao wapewe vyakula hivyo na pia sabuni ya kuwasaidia kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.Alisema wagonjwa wengi wa ukimwi wameacha kuhudhuria kliniki zao, jambo ambalo ni hatari kwa afya yao.

“Tumeshuhudia idadi chache ya wagonjwa wa ukimwi katika kliniki hii, nadhani imechangiwa na woga kuwa huenda wakapata maradhi ya Covid-19 au unyanyapaa,” akasema Dkt Awadh huku akipokea msaada huo.

Kulingana na ripoti ya Wizara ya Afya, maambukizi ya ukimwi yalipungua wakati wa janga la corona, lakini hofu kubwa ni kuwa maradhi ya covid-19 ni hatari kwa wagonjwa wa ukimwi.

You can share this post!

ODM kutumia kura ya maoni kupata mgombea ubunge

Sheria za vyama vya ushirika zibadilishwe, wasema wafugaji