• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 1:29 PM
Neymar na wachezaji wengine 4 walishwa kadi nyekundu PSG ikizikwa na Merseille

Neymar na wachezaji wengine 4 walishwa kadi nyekundu PSG ikizikwa na Merseille

Na MASHIRIKA

NEYMAR Jr alikuwa miongoni mwa wanasoka watano walioonyeshwa kadi nyekundu mwishoni mwa mechi ya Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) iliyoshuhudia Paris Saint-Germain (PSG) wakipokezwa kichapo cha 1-0 kutoka kwa Olympique Marseille.

Alipokuwa akiondoka uwanjani, Neymar alimweleza msaidizi wa refa kwamba kilichochochea vurugu mwishoni mwa gozi hilo ni matamshi yaliyoashiria ubaguzi wa rangi.

Florian Thauvin alifunga bao la pekee na la ushindi katika mchuano huo. PSG kwa sasa wamepoteza mechi mbili za ufunguzi wa kampeni mpya katika Ligue 1 kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 1984-85.

Leandro Paredes na Layvin Kurzawa walioingia ugani kuwajibikia PSG katika kipindi cha pili, na Jordan Amavi na Dario Benedetto wa Marseille walifurushwa uwanjani pamoja na Neymar.

Kwa usaidizi wa teknolojia ya VAR, refa alirejelea tukio zima lililochangia fujo uwanjani na kumwonyesha Neymar kadi nyekundu baada ya kubaini kwamba alikuwa amempiga ngumi mchezaji wa Marseille.

Baada ya mchuano, Neymar aliandika kwenye mtandao wake wa kijamii kwamba “cha pekee anachojutia” ni kwamba hakutandika usoni Alvaro Gonzalez wa Marseille na badala yake akapiga tu kisogo cha beki huyo raia wa Uhispania.

Akimjibu Neymar kupitia mtandao wake wa kijamii, Gonzalez alisema: “Hakuna nafasi kwa wanasoka kubaguana kwa misingi ya rangi”.

Hoja ya Gonzalez ilisisitizwa na kocha Andre Villas-Boas wa Marseille aliyepinga kuwepo kwa kisa chochote kilichoashiria ubaguzi wa rangi miongoni mwa wachezaji wakati wa mechi hiyo iliyosakatiwa ugani Parc des Princes.

Mechi hiyo iliyohudhuriwa na takriban mashabiki 5,000 ilitawaliwa na hisia kali tangu mwanzo. Jumla ya kadi 17 za manjano zilitolewa na hiyo ikawa rekodi ya idadi kubwa zaidi ya kadi kuwahi kutolewa kwenye mchuano mmoja wa Ligue 1 katika karne hii ya 21.

Purukushani zilizoshuhudiwa mwishoni mwa kipindi cha pili zilianza baada ya Benedetto wa Marseille kumchezea visivyo Paredes, tukio lililomchochea kiungo huyo wa PSG kulipiza kisasi kwa kumrushia Benedetto ngumi kisha kumpiga Alvaro kwa kichwa.

Fujo ilizuka uwanjani baada ya Kurzawa kuanza kurushia makonde na mateke na Jordan Amavi wa Marseille. Benedetto na Paredes walionyeshwa kadi za pili za manjano huku Kurzawa wa Amavi wakifurushwa moja kwa moja kupitia kadi nyekundu.

Kabla ya VAR kubainisha kwamba Neymar alimpiga Alvaro, kulishuhudiwa tena patashika nyingine katika kipindi cha kwanza baada ya Alvaro kudai kwamba fowadi Angel Di Maria alikuwa amemtemea mate kimakusudi.

Di Maria na Neymar ni miongoni mwa wachezaji saba wa PSG waliougua ugonjwa wa Covid-19 hivi majuzi kabla ya msimu mpya wa 2020-21 katika Ligue 1 kuanza rasmi.

Ilikuwa mara ya kwanza tangu 2011 kwa Marseille kuwazidi PSG maarifa katika soka ya Ligue 1. PSG ambao ni mabingwa watetezi wa taji la Ligue 1, walipokezwa kichapo cha 1-0 na Lens katika mchuano wa ufunguzi wa Ligue 1 msimu huu. Miamba hao wa Ufaransa waliambulia nafasi ya 13 kwenye msimamo wa jedwali la Ligue 1 miaka 36 iliyopita baada ya kupoteza mechi mbili za kwanza za msimu wa 1984-85.

Mara ya mwisho kwa PSG kupoteza mechi mbili za kwanza za msimu bila kufunga bao ni 1978.

Mechi dhidi ya Marseille ilikuwa ya tatu kwa PSG kupoteza kwa 1-0. Mabao ya Benedetto na Di Maria hayakuhesabiwa kwa kuwa walitikisa nyavu baada ya kuotea. Chini ya kocha Thomas Tuchel, kikosi hicho kilipokezwa pia kichapo sawa na hicho kutoka kwa Bayern Munich kwenye fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Agosti 23.

TAFSIRI: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Mwanaharakati ajifunga mnyororo kwenye mnara wa Dedan...

Ulinzi Warriors wasajili wanavikapu wawili