Habari Mseto

Dalili serikali itafungua shule mwezi Oktoba

September 14th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

NA FAITH NYAMAI

UWEZEKANO wa shule, taasisi za elimu na vyuo vikuu kufunguliwa mwezi ujao wa Oktoba unazidi kuongezeka baada ya Waziri wa Elimu, Prof George Magoha kufichua kuwa wizara yake inawazia kubadilisha mpango wa shughuli za masomo kurejelewa Januari mwakani.

Prof Magoha jana aliamrisha jopo lililoteuliwa kuandaa mwongozo mpya wa kutoa mwanga kuhusu kufunguliwa kwa shule kutafakari kubadilisha tarehe za awali huku idadi ya maambukizi ya virusi vya corona ikizidi kupungua nchini.

Shule, vyuo na taasisi za elimu zilifungwa nchini mnamo Machi 16, siku tatu baada ya kisa cha kwanza cha virusi vya corona kuripotiwa nchini.

Wakati wa mkutano wa jana ambao ulihusisha wadau wa sekta ya elimu, Prof Magoha pia aliagiza vyuo vikuu na vile vya kiufundi vianze kufunguliwa kwa awamu.

“Niliitisha mkutano wa leo ili kushauriana na wanakamati wa jopo na wadau katika sekta ya elimu ili waanze kuandaa mwongozo mpya wa shughuli za masomo kurejelewa. Kutakuwa na kongamamo kuu jumuishi litakalofanyika Septemba 25 kutoa mwelekeo kuhusu suala hili,” akasema Prof Magoha katika Taasisi ya Ukuzaji Mtaala ya Kenya (KICD).

Wakati wa mkutano huo ambao ulichukua zaidi ya saa tatu, waliohutubu walipendekeza shule zifunguliwe mwezi ujao.

Kuhakikisha hilo linatimia, mwenyekiti wa jopo la elimu kuhusu Covid-19, Bi Sarah Ruto alipewa muda wa wiki moja na wanachama wenzake ili waibuke na mikakati maridhawa itakayopisha ufunguzi wa shule na kuishauri wizara hiyo jinsi ya kuitekeleza.

Mmoja wa waliohudhuria mkutano huo ambaye hakutaka anukuliwe, alifichulia Taifa Leo kwamba Prof Magoha aliviruhusu vyuo vikuu na vile vya kiufundi vianzishe ufundishaji wanafunzi wa moja kwa moja darasani.

“Waziri alivipa mamlaka vyuo vikuu viamue ni lini vyuo vyao vitafunguliwa rasmi kwa kuwa masomo yamekuwa yakiendelea kupitia mitandaoni kwa muhula wa kati ya Septemba na Desemba,” akasema.

Prof Magoha pia alipuzilia mbali madai kwamba fedha za kuwalipa walimu walioajiriwa na bodi za shule (BOM) bado hazijafika shuleni, akisisitiza pesa hizo zilitolewa wiki sita zilizopita.

“Yeyote anayesema pesa za walimu wa BOM hazijatolewa wanafaa wawaeleze wanakotoa habari hizo. Walimu wote ambao tulinakili taarifa zao muhimu wameshalipwa,” akasema.

Kwa sasa, alifichua wizara yake inaendelea na mchakato wa kutoa fedha nyingine kwa wafanyakazi wa shule na wanaosimamia shughuli ambazo zitasaidia kurahisisha ufunguzi wa shule.

Haya yanatokea huku baadhi ya walimu wakuu wakiendelea kulalamika kwamba fedha za kugharimia miradi mbalimbali kwa maandalizi ya ufunguzi wa shule, bado hazijawafikia.

Waliohudhuria mkutano wa jana ni maafisa wa wizara, wale wa vyama vya Knut na Kuppet, wanachama wa Muungano wa Walimu Wakuu wa Shule za Upili (KESSHA) na wenzao wa Shule za Msingi (KEPSHA,), Chama cha Wazazi na wanachama wa Uasu.

Wiki ijayo, Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i na mwenzake wa Afya, Bw Mutahi Kagwe wanatarajiwa kuongoza kongamano kuu litakalotoa mwelekeo kuhusu jinsi Wakenya watakavyorejelea maisha yao ya awali kwa kuzingatia masharti ya kuzuia kuenea kwa corona.