Habari Mseto

Maskwota wa Nguu Tatu wafanya maandamano hadi kwa afisi ya mbunge

September 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MISHI GONGO

MASKWOTA katika mtaa wa Nguu Tatu eneobunge la Kisauni mjini Mombasa waliandamana hadi kwa afisi ya mbunge wa Kisauni Ali Mbogo kumtaka awasaidie kupata kipande chao cha ardhi.

Maskwota hao ambao ni zaidi ya 3000 walikuwa wamejawa na ghadhabu na walikita kambi nje ya afisi ya mbunge huyo wakisema kuwa hawatabanduka hadi pale mbunge huyo atakapokubali kusikiliza malalamishi yao.

Walibeba vyombo vyao, meko na hata magodoro wakisema kuwa wako tayari kulala eneo hilo hadi watakaposikizwa.

Mkazi wa eneo hilo Bw Robert Lugo alisema mabwenyenye wamekuwa wakiwahangaisha kwa muda mrefu.

“Tumekuwa hapa kwa sababu mbunge huyu aliahidi kuja katika shamba hilo kuzungumza nasi lakini hajafika,” akasema.

Alisema kesi ya mzozo huo tayari iko mahakamani lakini mabwenyenye wanaendelea kukiuka amri ya mahakama.

“Mahakama ilitoa agizo ya sisi kutofurushwa wala kujengwa ukita lakini tayari wamejenga ukuta wa futi tisa na lango. Tumeamua hatutaondoka hapa hadi mbunge wetu aje atupe mwelekezo,” akasema.

Mwengine Bi Mbodze Mwambaji alisema maafisa wa polisi wanawahangaisha katika eneo hilo.

“Kuna maafisa wa polisi ambao wanalinda lango,tukitaka kutoka nje wanatuambia tusirudi,” akasema.

Alisema ardhi hiyo ni ya ukubwa wa ekari 383.

Alieleza kuwa walipeleka kesi hiyo katika mahakama ya Shanzu mwaka 2017 na mahakama hiyo ikaagiza maskwota hao kugawanya shamba hilo na kampuni ya kutengeza maziwa ya Hussein Dairy ambaye anaaminika kuwa mmiliki.

Alisema licha ya agizo hilo wamiliki wapya wamejitokeza kudai umiliki na tayari wameanza kujenga ukuta.

“Sasa Bandari Sacco imekuja kudai umiliki. Wameanza kujenga ukuta licha ya kukatazwa na mahakama,” akasema.

Maskwota hao waliilaumu Kaunti ya Mombasa kwa kile walidai ni “kunyakuwa vipande vya ardhi vya wanyonge”.

“Wengi wetu ni wafanyabiashara wadogowadogo na hatuna pahala pa kwenda hivyo tunaomba msaada wa serikali,” akasikika mmoja akisema kwa niaba yao.