Malala azimwa kwenda Ikulu
Na CHARLES WASONGA
SAA chache baada ya Seneta wa Kakamega Cleophas Malala kububujikwa machozi mbele ya wenzake na wakuu wa usalama akidai makachero wanalenga kumuua, Ikulu ilikosa kumwalika katika mkutano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na uongozi wa seneti.
Hii ni licha ya kwamba Bw Malala ni Naibu Kiongozi wa Wachache.
Jumanne, Septemba 15, asubuhi Rais Kenyatta alifanya mkutano uongozi wa mirengo yote miwili katika seneti kujaribu kutanzua mvutano ulioko kuhusu mfumo wa ugavi wa fedha kwa kaunti.
Walialikwa katika mkutano huo ni Kiongozi wa Wengi Samuel Poghisio, naibu wake Fatuma Dullo. Kiranja wa Wengi Irungu Kang’ata na naibu wake Farhiya Ali. Vile vile alikuwepo Kiongozi wa Wachache James Orengo, Kiranja wa Wengi Mutula Kilonzo Junior na naibu wake Beatrice Kwamboka.
Mkutano huo ulifanyika wakati ambapo Spika wa Seneti Kenneth Lusaka aliongoza mkutano wa Kamati ya Kuratibu Shughuli za Seneti kupanga kikao cha alasiri kujaribu kupata suluhu kuhusu suala hilo ambalo limegawanya seneti kuwili.
Mnamo Jumatatu, Bw Malala alidai kuna kikosi fulani cha maafisa wa upelelezi ambao wanalenga kumuua kutokana na msimamo wakati kuhusu suala hilo la mfumo wa ugavi wa fedha kwa kaunti.
“Mimi ni baba, mume na mwakilishi wa watu wa Kakamega, Inavunja moyo kwamba kuna maafisa au watu fulani kuketi mahala fulani kupanga kuniua. Nimesema mara sio moja kwamba maisha yangu yamo hatarini,” Bw Malala akasema huku akiangua kilio.
Inspekta Jenerali Hillary Mutyambai na Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti walikuwa wamefika katika kikao hicho kwenye ukumbi wa County, Nairobi, kutoa maelezo kuhusu malalamishi kuhusu usalama yaliyoibuliwa na Malala pamoja na maseneta wengine.