• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Kaunti zitaongezewa Sh50 bilioni kwa bajeti – Uhuru

Kaunti zitaongezewa Sh50 bilioni kwa bajeti – Uhuru

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta mnamo Jumanne, September 15, 2020, aliahidi kuwa Serikali ya Kitaifa itaongeza mgao wa fedha kwa kaunti kwa kima cha Sh50 bilioni katika mwaka wa kifedha wa 2021/2022 kama hatua ya kupiga jeki ugatuzi.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa utekelezaji wa nyongeza hiyo utategemea iwapo uchumi wa nchi utaimarika kufikia mwaka huo baadhi ya kuathirika na janga la Covid-19.

Rais Kenyatta alisema hayo katika mkutano aliotisha katika Ikulu ya Nairobi pamoja na maseneta wanaoshikilia nyadhifa za uongozi katika Seneti. Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Kiongozi wa ODM Raila Odinga na Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) Wycliffe Oparanya.

“Mkutano huo uliamua kwa kauli moja kwamba kwa kutegemea hali ya uchumi, serikali katika mwaka wa kifedha wa 2021/2022 itajizatiti kutenga Sh50 bilioni zaidi kwa Serikali kama njia ya kuimarisha ugatuzi,” ikasema taarifa kutoka kitengo cha habari za rais (PSCU).

Inaonekana kuwa Rais Kenyatta alitoa pendekezo hilo kama njia ya kuwashawishi maseneta kupitisha mfumo mpya wa ugavi wa fedha kwa kaunti ambao umepingwa na maseneta kutoka kaunti 18. Kaunti hizo ni zile ambazo zitapoteza fedha endapo mfumo huo utatekelezwa. ambazo zinakadiriwa kufika Sh17 bilioni.

Kufuatia ahadi hiyo ya nyongeza ya fedha kwa kaunti, Rais Kenyatta aliwahimiza maseneta kumaliza mvutano kuhusu mfumo huo wa ugavi wa fedha, ili kuwezesha serikali 47 za kaunti kusambaziwa Sh316.5 bilioni zilizotengewa mwaka katika bajeti ya mwaka huu.

Seneti iliwakilishwa katika mkutano huo na Samuel Poghisio (Kiongozi wa Wengi), Irungu Kang’ata (Kiranja wa Wengi), Fatuma Dullo (Naibu Kiongozi wa Wengi na James Orengo (Kiongozi wa Wachache).

Wengine walikuwa Naibu Kiranja wa Wengi Farhiya Ali, Kiranja wa Wachache Mutula Kilonzo Junior, Naibu Kiranja wa Wengi Beatrice Kwamboka na Seneta wa Taita Taveta Johannes Mwaruma.

You can share this post!

Malala azimwa kwenda Ikulu

Vikosi vya Kenya Cup vyafutilia mbali mpango wa kukamilisha...