Mbunge apinga Badi kujumuishwa kwa Baraza la Mawaziri
Na JOSEPH WANGUI
MBUNGE wa Kandara, Bi Alice Wahome ameenda mahakamani kupinga hatua ya Rais Uhuru Kenyatta kumjumuisha Mkurugenzi wa Shirika la Huduma za Jiji la Nairobi (NMS), Meja Jenerali Mohammed Badi katika Baraza la Mawaziri.
Bi Wahome anataka Mahakama iamue kwamba hatua hiyo ya Rais ni kinyume cha sheria na inakiuka Katiba, hivyo basi ibatilishwe.
Kwenye kesi aliyoiwasilisha katika Mahakama Kuu akiitaja kuwa suala la dharura, Bi Wahome ambaye ameonekana kuwa mkosoaji mkuu wa mrengo wa Rais Kenyatta, anasema hakuna sheria ndani ya Katiba inayoruhusu kuteuliwa kwa Jenerali Badi kwenye Baraza la Mawaziri.
Anasema kwa kumteua Jenerali wa kijeshi kukaa kwenye vikao vya mawaziri, Rais aliruhusu ‘mgeni asiyetambuliwa’ kushiriki kwenye uamuzi muhimu wa masuala ya nchi, jambo analoamini kuwa si halali.
“Vitendo vya Rais kumjumuisha mtu kama huyo kwenye baraza la mawaziri ni ukiukaji wa katiba na havifai. Jinsi ambavyo Baraza la Mawaziri lipo kwa sasa ni kinyume na Katiba na halikubaliki,” akasema kwenye malilio yake kwa maahakama.
Kulingana naye, mashtaka yake yanaibuaa masuala mazito kuhusu kuundwa kwa serikali na taasisi zake, kwa njia ambayo ni mbali na ile inayotakiwa kikatiba.
“Meja Jenerali Badi amepenyezwa katika Baraza la Mawaziri bila ya kufuata kanuni zilizowekwa na katiba. Serikali sasa imeundwa kwa njia ambayo haikubaliki kisheria,” anasema na kuongeza kwamba kuteuliwa kwa mwanajeshi huyo hakutambuliwi na sheria za nchi.
Pia anamkosoa Rais Kenyatta kwa uteuzi huo wa moja kwa moja bila ya kushirkikisha Bunge kama inavyohitajika na Kifungu cha 152(2).
Kifungu hicho kinasema, “Rais atapendekeza, na kwa idhini ya Bunge, atateua Waziri.”
Bi Wahome anasema uaamuzi wa kumjumuisha Meja Jenerali Badi bila ya kupigwa msasa na kujua tabia yake miongoni mwa masuala mengine, ni ukiukaji wa kifungu cha 95(5) cha Katiba kinachohitaji mawaziri wapigwe msasa na Bunge kabla ya kuapishwa.
Kulingana na kifungu hicho cha 95(5)(5) Bunge linapewa mamlaka ya mwisho kukagua tabia na mienendo ya mtu aliyeteuliwa kuhudumu katika Afisi ya Rais, Naibu Rais, na maafisa wengine wa serikali.
Bunge ndilo lenye mamlaka ya kufuatilia utendakazi wa taasisi za serikali na lina wajibu wa kuanzisha mchakato wa kuwaondoa maafisa hao iwapo kutakuwa na ukiukaji wowote wa sheria au sababu nyingine zinazokubaliwa na katiba.
Kupitia kampuni ya mawakili ya Gitonga Mureithi and Company Advocates, mbunge huyo anasisitiza ni ukiukaji wa katiba kumlisha Meja Jenerali Badi kiapo cha Siri mnamo Septemba 10 mwaka huu.
Meja Jenerali Badi alilishwa kiapo cha Siri, ambayo ni mojawapo ya masharti ya watu wote wanaohudhuria vikao vya Baraza la Mawaziri au kushiriki katika shughuli za baraza hilo.
Baadaye, Rais Kenyatta alitoa Agizo Nambari 3 la mwaka 2020 kujulisha umma kuhusu mabadiliko hayo na kuidhinisha rasmi kushiriki kwa Meja Jenerali Badi kwenye Baraza la Mawaziri.
Bi Wahome alisema amechukua hatua hiyo anayoamini wajibu wake kama mbunge haukuzingatiwa wakati wa kufaulisha mchakato wa kumuongeza Meja Jenerali Badi kwenye Serikali.