• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 4:48 PM
Mashabiki wa Gor wakejeli washambuliaji kwa kufuma mabao hewa

Mashabiki wa Gor wakejeli washambuliaji kwa kufuma mabao hewa

Na GEOFFREY ANENE

MASHABIKI wa Gor Mahia wamelia sana kuhusu ubutu wa washambuliaji wao mbele ya lango baada ya klabu hiyo kukabwa 0-0 na USM Alger katika mechi ya pili ya Kundi D ya Kombe la Mashirikisho, Jumatano.

Baada ya mechi hiyo iliyochezewa katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani jijini Nairobi, mashabiki walilaumu sana washambuliaji na hata kupendekezea kocha Dylan Kerr wazo la kuimarisha kikosi kwa kusajili washambuliaji. Lawama kubwa ilielekezwa kwa raia wa Ivory Coast Ephrem Guikan.

Shabiki Kassusy Judy Jeff alisema, “Safu ya mbele Bwana Kerr…”

Naye Apong Kor, “Guikan anahitaji kuchukulia kazi yake kwa uzito. Atafanya Gor ijute sana (kupoteza nafasi nyingi)! “Nilimtazama na kulalamika wakati wa mechi ya kirafiki dhidi ya Hull City (Mei 13). Anafaa kutemwa mapema.”

Davvy Robberto Starboy, “Guikan ni butu kabisa.” Benard Awright, “Huyu mchezaji anaitwa Guikan siwezi kumtazama tena akivalia jezi ya Gor. Hafai kuvaa jezi hiyo, hawezi kutumia nafasi nyingi anazopata, tukiendelea kuandikisha sare, tutajipata tukivuta mkia kwenye kundi letu.”

Naye Tarzan Johnso alisema, “Gor ilicheza mechi safi…shida yetu kubwa ni safu ya mbele…(washambuliaji wetu) hawawezi kukamilisha hata nafasi rahisi…mambo yalikuwa hivi dhidi ya Esperance (Tunisia), Rayon Sport (Rwanda), Hull City (Uingereza) na sasa USM Alger…tunahitaji (kununua) mshambuliaji…(Jacques) Tuyisenge, Guikan na (Meddie) Kagere hawana utulivu…tusipobadilika, hatutaenda mbali.

Soka ni mchezo wa kutumia nafasi zako vyema. Hata hivyo, natofautiana na wengi wanaolaumu Guikan. Nadhani alicheza vyema. Tuyisenge ndiye alipoteza nafasi nyingi na alikuwa butu.”

Marefa pia hakuponea hasira ya mashabiki. Kevin Gama Pintoh alisema,” Hii ndiyo sababu marefa wengine wanatiwa adabu… Hata hivyo, naomba mmpeleke Guikan katika klabu nyingine kwa mkopo kwa sababu bado anakosa ujuzi wa kupita mabeki. Tafadhali (Gor) tafuteni mvamizi kutoka Misri kwa sababu wana kasi na nguvu kukabili mabeki na kusababisha bao la kujifunga ama penalti.”

Gor imesalia katika nafasi ya pili kwenye kundi lake kwa alama mbili. Kabla ya sare tasa dhidi ya Alger, Gor ilikuwa imekabwa 1-1 dhidi ya Rayon nchini Rwanda.

Alger inaongoza kwa alama nne. Ilipepeta Young Africans ya Tanzania 4-0 nchini Algeria katika mechi ya kwanza. Rayon ina alama mbili nayo Yanga inavuta mkia kwa alama moja. Mechi ijayo ya Gor ni dhidi ya Young Africans hapo Julai 18 nchini Kenya.

You can share this post!

Huenda City Hall ikaadhibiwa vikali na Kenya Power

Kigali Peace Marathon yavutia watimkaji 8,000

adminleo