LISHE: Namna ya kuandaa mboga mchanganyiko
Na MARGARET MAINA
Muda wa kuandaa: Dakika 10
Muda wa kupika: Dakika 15
Walaji: 2
MBOGA za majani zina faida nyingi za kiafya.
Hii ni kutokana na asili yake ya kuwa na vitamini kwa wingi, madini kwa wingi; na dawa zinazotokana na mimea kwa kulinda afya.
Mboga za majani pia zinasaidia kukinga mwili dhidi ya magonjwa mbalimbali.
Vile vile husadia kupunguza, kurekebisha na kuweka uzani sawa.
Vinavyohitajika
• pilipili mboga 3 za rangi tofauti
• bamia
• karoti
• vitunguu maji
• mafuta ya kupikia
• chumvi
Maelekezo
Kata kitunguu. Weka kwenye chombo kando.
Kata karoti.
Osha bamia, kata na kisha weka kando.
Weka sufuria au kikaangio mekoni. Ongeza mafuta na acha yapate moto.
Weka kitunguu, koroga kiasi. Ongeza bamia endelea kukoroga. Kisha funika ili viive kwa muda.
Weka pilipili mboga; koroga ili vichanganyike vizuri.
Ongeza karoti na uchanganye.
Sasa nyunyuzia chumvi kiasi na kisha koroga ili ienee na kukolea vizuri.
Funika mchanganyiko kwa muda wa dakika 10.
Acha chakula hiki kichemke vizuri huku ukigeuza kidogo na kisha funika tena kwa muda wa dakika tano.
Pakua na chakula unachopenda.