Familia yaililia serikali iwasaidie kusaka mpendwa wao aliyetoweka
Na DIANA MUTHEU
KWA mwezi mmoja sasa, Bi Regina David, 38 anasema kuwa hajajaliwa kupata usingizi mzito akiwaza ni wapi mumewe yuko, baada ya kutekwa nyara.
Akizungumza na Taifa Leo Dijitali nje ya majengo ya shirika la kutetea haki za binadamu la Haki Afrika mnamo Jumanne jioni, Bi David alisema kuwa mumewe, Bw David Taitumu alitoweka mnamo Agosti 14, na mwezi mmoja umekamilika na hawajui alipo.
Bi David alisema kuwa alijaribu kumpigia mumewe simu siku hiyo lakini haikupokelewa, jambo ambalo lilimtia wasiwasi.
“Haikuwa kawaida yake kulala nje, lakini mnamo Agosti 14 hakurudi nyumbani. Tulimsubiri kwa muda mrefu na baada ya kumpigia simu ambayo haikupokelewa, niliwaita ndugu zake na sote tulianadamana hadi kituo cha polisi cha Central, Mombasa mnamo Agosti 15, kuandikisha ripoti. Baadaye gari lake lilipatikana karibu na shule ya msingi ya Mombasa, karibu na eneo la Lighthouse alipokuwa amezoea kujivinjari na wenzake wakitafuna miraa,” akasema Bi David.
kulingana na Bi David, mumewe alitekwa nyara mwendo wa saa moja jioni katika eneo la lighthouse, karibu na bustani la Mama Ngina, sehemu aliokuwa amezoea kutafunia miraa pamoja na wenzake.
“Baadhi ya mashahidi walitueleza kuwa mume wangu alizuiliwa na magari mawili katika eneo la lighthouse, Mombasa, moja mbele na lingine nyuma. Watu sita wasiojulikana, waliokuwa wamejihami walitoka katika magari hayo na kumlazimisha ashuke kutoka kwa gari lake. Alikataa, hivyo wakalazimika kukivunja kioo cha gari yake na kumtoa nje, wakamwingiza katika gari lao moja na kuliendesha kwa kasi,” akasema.
Bi David alisema kuwa gari lao lilipatikana limeegeshwa karibu na shule ya msingi ya Mombasa ambalo haliko mbali sana na eneo la Lighthouse, ambako kisa hicho kilitendeka.
“Tulipoandikisha ripoti chini ya OB13/15/8/2020 katika kituo hicho, polisi walianza uchunguzi na walilipata gari letu. Tulipoenda kuliangalia gari hilo, tulipata kuwa kioo cha gari hiyo aina ya premio yenye nambari ya usajili KBE 958V na rangi ya fedha, kilikuwa kimevunjwa upande wa dereva. Hata hivyo, vifunguo vya gari hiyo vilikuwa ndani ya gari hiyo,” akasema Bi David huku akiongeza kuwa shahidi mmoja alisema kuwa baada ya David kuchukuliwa na watu hao, mmoja miongoni mwao alirudi na kuliendesha gari hilo hadi sehemu ambalo lilipatikana limeegeshwa.
Akiwa mwingi wa majonzi, Bi David alisema kuwa hawakuweza kumpata mumewe hata baada ya kumtafuta katika hospitali na jela zote katika kaunti ya Mombasa.
Alisema kuwa maisha yamekuwa magumu ikizingatiwa kuwa walimtegemea mumewe kwa kila kitu.
Bi David aliilaumu idara ya polisi kwa kuchukua muda mwingi kufanya uchunguzi, bila ya kuijulisha familia hiyo alipo mpendwa wao.
“Alikuwa na biashara zake halali ambapo anamiliki duka mbili za rejareja na nyumba za kukodisha eneo la Bamburi na Likoni, na kama kuna makosa alifanya, heri akamatwe kama Mkenya mwenye haki na afikishwe mahakamani. Mwezi mmoja umeisha na polisi wanasema kuwa bado wanafanya uchunguzi, lakini hatuna habari zozote kuhuzu aliko,” akasema Bi David.
Mwanawe Bw Taitumu, Bi Sylvia Kagendo, mwenye umri wa miaka 19 aliiomba serikali kuingilia kati na kuhakikisha kuwa babake ametafutwa na kurejeshwa nyumbani.
“Shule zinakaribia kufunguliwa na lazima karo itatakikana. Mimi ni mwanafunzi wa chuo kikuu na ninamtegemea babangu anilipie karo. Pia, nina binamu ambaye anamtegemea,” akasema Bi Kagendo.
Kakake mwathiriwa, Bw Phineas Kirimi alidai kuwa walijaribu kutuma ujumbe kwa simu ya nduguye mnamo Agosti 18 kutumia mtandao wa Whatsapp, na ujumbe huo ulipokelewa mnamo Agosti 19.
“Tulishangaa kuwa ujumbe huo ulipokelewa, kumaanisha kuwa kuna mtu ambaye alikuwa akiitumia simu ya kakangu. Pia, iwapo maafisa wa polisi walikuwa wamejitolea kumtafuta ndugu yangu, wangefuatilia ni wapi simu yake ilikuwa manake ilikuwa haijazimwa kwa siku mbili mfululizo tangu atekwe nyara,” akasema huku akiongeza kuwa hawatachoka kumtafuta Bw Taitumi.
“Hatujawahi kusikia kuwa anafanya biashara za magendo wala ameshikwa na maafisa wa polisi. Hata kama pengine aliwahi kuhusika katika vitendo fulani haramu, ambavyo hatuvijui, mbona wasimkamate na kumpeleka mahakamani?” akauliza Bw Kirimi.
Bw Kirimi aliwaomba maafisa wa polisi katika kaunti ya Mombasa kutafuta kamera za usalama maarufu CCTV katika eneo ambalo kisa cha utekaji nyari kilitendeka, na waweze kuwafuatilia na kuwakamata washukiwa.
Mkurugenzi wa Haki Afrika, Hussein Khalid aliziomba idara husika ziingililie kati na kuhakikisha kuwa visa vya watu kupotea kiholelaholela vinakomeshwa eneo la Pwani.
Bw Khalid alisema kuwa kulingana na takwimu zao, watu 19 wameweza kupotea ovyo wasijulikane walipo mwaka huu, lakini miongoni mwao sita waliweza kupatikana.
“Kama mtu amefanya makosa, basi akamatwe kiungwana kulingana na sheria na katiba ya Kenya, kisha afikishwe mahakamani. Visa vya watu kupotea ovyo vimeongezeka sana katika eneo la Pwani na ni jambo ambalo serikali inafaa kuangazia kwa makini,” akasema Bw khalid.