Siasa

Maseneta wamkaanga Oparanya kwa amri yake ya kufunga kaunti

September 17th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na CHARLES WASONGA

MASENETA Jumatano walimshambulia mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) Wycliffe Oparanya kwa cheche za maneno kufuatia tangazo lake kwamba kaunti zitasitisha huduma kwa wananchi kuanzia Alhamisi.

Viongozi hao walimtaja Bw Oparanya kama msaliti, mwongo na ambaye anaongoza “kundi cha watu” ambao wanalenga kuhujumu kazi ya seneti ya kutetea ugatuzi..

Maseneta walisema ni wakati wa hatamu ya uongozi wa Gavana huyo wa Kakamega ambapo CoG imekuwa ikishirikiana na Serikali Kuu na hivyo kuwasaliti maseneta ambao wamekuwa wakipigania nyongeza ya mgao wa fedha kwa serikali za kaunti.

“Nitamwambia Gavana wangu Kivutha Kibwana tutamng’oa mamlakani akithubutu kufunga Hospitali ya Makueni Level 4. Ni makossa makubwa kwa gavana yeyote kutii amri ya gavana mwenzake ya kufungwa hospitali,” akasema Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Junior.

Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula alisema hatua hiyo ya kusitisha shughuli za kaunti ni kielelezo cha matumizi mabaya ya mamlaka.

Kiongozi huyo wa Ford Kenya alieleza kuwa CoG sio mwajiri wa wafanyakazi katika kaunti na hivyo haina mamlaka ya kuwapa likizo ya wiki, mbili alivyoagiza Bw Oparanya katika taarifa yake.

“Magavana hawawezi hata kumtuma likizo mfanyakazi wa kudumisha usafi. Mwenyekiti wa baraza la magavana hafai kujipa mamlaka ambayo hana, huku akiwatusi maseneta anavyotaka,” Wetang’ula akasema.

Naye Seneta wa Kitui Enock Wambua alisema Bw Oparanya amebuni mwenendo mbaya wa kutoa taarifa za kukera.

“Alitoa taarifa za kiajabu alipofika mbele ya Kamati ya muda ya Seneti iliyochunguza Sakata ya Mpango wa Ukodishaji Vifaa vya Kisasa vya Kimatibabu (MES),” akasema.

Bw Wambua alisema ni baada ya mvutano wa sasa kuhusu mfumo wa ugavi wa fedha baina ya kaunti umechangiwa na hatua ya Bw Oparanya kukubaliana na Serikali ya Kitaifa kwamba kaunti zitengewe Sh316.5 bilioni mwaka huu, sawa na mgao wa mwaka jana.

“Oparanya anataka kaunti kama vile Wajir, Mandera, Kilifi na zinginezo ziendelea kubaguliwa na kwa kutengewa fedha finyu kwa sababu anaendeleza ukuruba na Serikali Kuu,” akasema.

Seneta wa Narok Ledama Ole Kina alisema CoG haina mamlaka ya kufunga kaunti yoyote kwa sababu ni asasi ambayo haitambuliwi katika Katiba.

“Ukimteua mtu kuwa kiranja, anasahau kuwa angali mwanafunzi,” akasema Ole Kina huku mwenzake wa Migori Ochillo Ayacko akimtaja Bw Oparanya ni “jambazi”.

Gavana Oparanya alikuwa amefika mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Covid-19 kwa njia ya mtandao. Kamati hiyo inayoongozwa na Seneta Maalum Sylvia Kasanga inachunguza sakata ya ununuzi wa vifaa vya matibabu katika Mamlaka ya Ununuzi wa Dawa na Vifaa vya Matibabu (KEMSA).

Maseneta hao walimkaripia Gavana huyo wa Kakamega saa chacha baada ya yeye kuamuru kusitishwa kwa huduma na magavana wawape wafanyakazi likizo ya majuma mawili kutokana na mvutano unaoendelea katika seneti kuhusu mfumo wa ugavi wa fedha baina ya kaunti

Baadhi ya huduma zitakazoathirika ni zile za afya kwani wagonjwa wanaotaka huduma za malazi hawashughulikiwa kwani ni zile za wagonjwa kutibiwa na kwenda nyumbani pekee zitatolewa.

Hii ni baada ya maseneta Jumanne, Septemba 15, kukosa kuelewana kwa mara ya 10 kuhusu mfumo mwafaka wa ugavi wa Sh316.5 bilioni zilizotengewa serikali katika mwaka huu wa kifedha wa 2020/2020.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari mwenyekiti wa CoG alielezea kukerwa na hali kwamba “bado haijulikani ni lini mvutano kuhusu suala hilo utatatuliwa.”

“Serikali zote za kaunti zinashauriwa kutoa ilani kwa wafanyakazi kwamba watapewa likizo ya wiki mbili na huduma zote zisizo muhimu zitasitisha. Na hospitali zote hazitawapokea wagonjwa wa kulazwa. Ni huduma chache tu za wagonjwa kutibiwa na kwenda nyumba zitatolewa,” Bw Oparanya, ambaye ni Gavana wa Kakamega, akasema.

Hata hivyo, mwenyekiti huyo wa CoG alimshukuru Rais Uhuru Kenyatta kwa kuahidi kuongeza mgao kwa kaunti kwa kima cha Sh50 bilioni katika mwaka wa kifedha ujao wa 2021/2022.

Mnamo Septemba 3, 2020 Bw Oparanya alisema kwamba seneti imekwamisha shughuli katika serikali za kaunti kwa kufeli kuelewana kuhusu mfumo wa ugavi wa mapato kwa kaunti ndiposa kaunti zisambaziwe sehemu ya mgao wao wa fedha Sh316.5 bilioni.

Gavana huyo alisema hatua ya Seneti kufeli kukubaliana kuhusu mfumo huo umechangia serikali za kaunti kushindwa kulipa mishahara ya wafanyakazi, wakiwemo wahudumu wa afya.

“Kwa hivyo tunatoa onyo kwa seneti kwamba ombi la kuivunjilia mbali inaweza kuwasilishwa na mwananchi yeyote kupitia mahakama kuu kulingana na kipengele cha 258 cha Katiba,” akasema.