• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 2:55 PM
Raila Junior akemea marafiki wa baba yake

Raila Junior akemea marafiki wa baba yake

Na JUSTUS OCHIENG

MWANAWE kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga, Raila Jnr (Pichani) amewakasirisha viongozi wa chama hicho kwa kuwataka kuzingatia ajenda za maendeleo kwa umma na demokrasia badala ya siasa duni.

Kwenye ujumbe wa Twitter mnamo Jumanne, Raila Jnr alikemea chama hicho na kukitaka kulenga kuwahudumia wananchi.

“Sisi kama ODM tunajitaji kurudi katika misingi yetu. Hatuko kwa ajili ya kuonyesha ndege za kibinafsi na warembo huku tukitukana wanasiasa wapinzani wetu. Tuna ajenda ya maendeleo iliyofafanuliwa wazi katika manifesto yetu. Tuzingatie kutoa huduma, kukuza demokrasia na kulinda haki za raia,” aliandika Raila Junior.

Kauli hii ilifuata aliyotoa Jumapili akimkosoa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa chama cha ODM, Junet Mohammed, ambaye ni mwandani wa karibu wa babake.

“Hakika ukiwa kiranja wa wachache bungeni na mbunge wa miaka mingi, Japo haukubaliani na kile alichosema Oscar Sudi unafaa kutetea haki yake ya kujieleza. Uhuru wa kujieleza ni nguzo ya demokrasia yetu,” Raila Jnr alimweleza Bw Junet kwenye ujumbe wa Twitter Jumapili.

Chama cha ODM chini ya uongozi wa Bw Odinga kimeonekana kupoteza mwelekeo kwa kupuuza jukumu lake la chama rasmi cha upinzani bungeni, na badala yake kinaunga mkono serikali kinayopasa kuwa kikitathmini utendakazi wake na kukosoa.

Mnamo Jumatatu, Kiongozi wa Narc-Kenya, Martha Karua alisema wabunge wa ODM wanapasa kuondoka kwenye kamati za bunge za kutathmini serikali kwa sababu hawatekelezi jukumu hilo.

Wabunge wa chama hicho na maseneta wamekuwa wakiunga mkono hatua za utawala wa Jubilee hata wakati ambapo zinakiuka Katiba, sheria na maslahi ya wananchi.

Ni kutokana na kuporomoka kwa misingi ya demokrasia ambayo chama hicho kilianzishwa juu yake ambapo Raila Junior amejitokeza kuongoza juhudi za kukifufua kulingana na matarajio ya wanachama wake.

Kauli zake ziliwachangamsha washirika wa Naibu Rais William Ruto huku Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wa akimtaka mwenyekiti wa ODM, John Mbadi kufuata ushauri wa Raila Jnr na kuruhusu chama chake kuzingatia ajenda za kunufaisha Wakenya.

Lakini Bw Mbadi aliyekuwa akizungumza katika runinga ya Citizen mnamo Jumanne, alisema kwamba Raila Jnr hazungumzi kwa niaba ya chama cha ODM.

“Siko katika mitandao ya kijamii lakini iwapo yeye Raila Jnr aliandika hayo kwenye Twitter, hazungumzi kwa niaba ya chama cha ODM. Ni mwanachama wa ODM lakini hashikilii wadhifa chamani. Ni mwana wa kiongozi wa chama chetu tu,” Bw Mbadi alisema.

Hata hivyo alisema sio mara ya kwanza Raila Jnr kuwa na misimamo tofauti kuhusu masuala kadhaa na ni haki yake kufanya hivyo.

“Hii haifai kutumiwa kama msimamo wa ODM. Misimamo ya ODM hutolewa na maafisa wa chama wakiongozwa na kiongozi wetu Raila Odinga,” Bw Mbadi alisema.

ODM kimekuwa kikikumbwa na mizozo ya ndani ambayo husababishwa na azma zinazokinzana baina ya viongozi.

You can share this post!

ONGAJI: Mashirika yameanika udhaifu wa sekta ya afya Afrika

Akana mke peupe kulinda wa pembeni