Makala

WANDERI: Tofauti za kidini zafaa zitatuliwe kwa utulivu

September 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

DINI ni mojawapo ya nguzo kuu ambazo humpa mwanadamu utambulisho maalum katika maisha yake.

Huwa kama kurunzi inayotoa mwanga kwenye safari katika msitu mkubwa nyakati za usiku.Dini vile vile ni msingi thabiti unaohusu maisha ya kila siku ya jamii husika.

Hivyo, uwepo na mchango wake kwenye maisha ya mwanadamu ni jambo ambalo halipaswi kupuuzwa hata kidogo.

Historia ya dini ni ndefu, kwani uwepo wake ulianza nyakati za uumba wa dunia.Licha ya umuhimu wake mkubwa, baadhi ya watu wamekuwa wakitumia visivyo kanuni na miongozo iliyopo ya kidini kujifaidi wao wenyewe.

Matokeo ya fasiri hizo za kupotosha huwa ni migongano isiyofaa ya kiimani, ambayo wakati mwingine hugeuka kuwa chemichemi za mafarakano, utengano na hata maafa.

Mfano halisi ni mgawanyiko unaolikumba dhehebu la Legio Maria katika eneo la Nyanza.Mnamo Jumatatu, makabiliano makali yalizuka kati ya pande mbili pinzani, zikizozania uongozi wa kanisa hilo.Kwa mujibu wa taarifa za polisi, watu wanane wamefariki kufikia sasa huku wengine wakijeruhiwa.

Mzozo huo unahusisha kambi za Papa Raphael Adika na mwenzake, Raphael Kalul.Ni mvutano ambao umekuwepo kwa muda mrefu, kiasi cha hata viongozi hao kwenda mahakamani kutafuta utatuzi kuhusu masuala tata yanayowakumba.

Cha kushangaza ni kuwa, licha ya mwingilio wa mahakama na taasisi zingine, juhudi hizo hazijafaulu.Kimsingi, mzozo huo umechora taswira isiyofaa kuhusu dini kama kioo cha jamii na chemichemi ya usuluhishi wa masuala tata yanayoikumba.

Ingawa dhehebu hilo si la kwanza kukumbwa na tofauti kama hizo, mwelekeo huu umekuwa ukishuhudiwa sana katika dini nyingi duniani, hali inayotia wasiwasi kuhusu nafasi na mchango wake katika jamii.

Kinyume na migawanyiko ya sasa, tofauti zilizoshuhudiwa awali kwenye madhehebu mbalimbali zilitoa nafasi kwa viongozi kukosoana na kujengana baina yao.

Mara nyingi, athari za mizozo iliyoshuhudiwa zamani zilikuwa ni ukuaji na mpanuko wa kimawazo kuhusu uongozi wa dini mbalimbali.

Kwa mfano, tofauti kali zilizozuka kati ya Martin Luther na Papa Leo wa Kanisa Katoliki ndizo zilimfanya kuanzisha kanisa la Lutheran Church mnamo 1517.

Kuanzishwa kwa kanisa hilo kulichangia mchipuko wa makanisa mengine yenye mitazamo huria kuhusu imani za Kikristo katika sehemu mbalimbali duniani.Hilo ndilo pia lilichangia kuanzishwa kwa vyuo vya kiusomi kuhusu masuala ya kidini katika dunia ya kale na kisasa.

Athari za vyuo hivyo zilikuwa ni uwepo wa Wamishenari, ambao walizuru Afrika na kuchangia sana katika ujenzi wa makanisa, ukuaji wa elimu, masuala ya afya kati ya mengine.

Mkondo uo huo ndio uliandama ukuaji wa dini ya Kiislamu kutoka chimbuko lake mjini Mecca, Saudi Arabia hadi duniani kote.

Bila shaka, ni wakati viongozi wa kidini kufahamu kwamba badala ya maafa, migawanyiko inayozuka kati yao inapaswa kutoa nafasi kwa ukuaji dini ama dhehebu husika.

[email protected]