• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Nyoro awahimiza wafanyabiashara kuunda vyama vya ushirika

Nyoro awahimiza wafanyabiashara kuunda vyama vya ushirika

Na SAMMY WAWERU

Wafanyabiashara Kaunti ya Kiambu wamehimizwa kubuni makundi na pia kujiunga na vyama vya ushirika (Sacco) ili waweze kupata mikopo inayotolewa na serikali.

Gavana James Nyoro amesema ni rahisi kwa wafanyabiashara kupewa mikopo wakiwa kwenye makundi au chama cha ushirika, ikilinganishwa na mtu binafsi.

Bw Nyoro alisema makundi hayo yanapaswa kusajiliwa chini ya idara husika, hatua itakayowawezesha kupewa fedha.

“Ninahimiza wafanyabiashara Kiambu waunde makundi na pia kujiunga na vyama vya ushirika, hatua ambayo itawawezesha kupata mikopo,” akasema gavana.

Akiwahimiza kujiunga na vyama ushirika, Nyoro alisema ni kati ya mbinu faafu kuweka akiba na kupata mikopo kwa njia rahisi.

Aidha, Bw Nyoro alisema akiba hiyohiyo ndiyo itawasimamia kupanua na kuimarisha biashara zao. “Ni muhimu wafanyabiashara wajiunge kwa makundi na kuleta pesa zao pamoja, waziweke kama akiba kwenye vyama vya ushirika. Mkusanyiko huo wa mapato utaimarisha na kustawisha jitihada katika bbiashara,” akashauri.

Mwezi uliopita, Agosti, gavana huyo wa Kiambu alikutana na wafanyabiashara wa soko la Githurai, waliokuwa wakichuuzia kandokando mwa reli na kuondolewa ili kuruhusu ufufuaji wa uchukuzi na usafiri wa garimoshi kati ya Nairobi na Nyanyuki unaoendelea.

Bw Nyoro alipiga jeki wafanyabiashara hao kwa kuwapa kima cha Sh2.5 milioni, kuanzisha chama cha ushirika kwa minajili ya kuimarisha kazi zao.

Kabla kujiunga na Sacco, ni muhimu kuthibitisha uhalisia wake ili kukwepa kutapeliwa. Vilevile, kwa wanaoanzisha vyama vya ushirika wanashauriwa kuvisajili katika idara husika.

  • Tags

You can share this post!

Neymar nje mechi mbili kwa utovu wa nidhamu

Maseneta wawapongeza Uhuru na Raila kwa kuokoa jahazi