Habari Mseto

Shule za kibinafsi zaomba msaada

September 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

Baadhi ya wamiliki wa shule za kibinafsi nchini wameiomba serikali kuwasaidia kuafikia mahitaji yanayotakikana ili kuruhusiwa kufungua shule.

Hata ingawa serikali haijatangaza wakati ambao shule zitafunguliwa, muonekano wa kupungua kwa maambukizi ya Homa ya virusi vya corona (Covid-19) nchini, Wizara ya Elimu imeashiria huenda zikafunguliwa hivi karibuni.

Shule zote na taasisi za elimu ya juu zilifungwa Machi 2020, kufuatia mkurupuko wa corona nchini.

Huku dalili zikionyesha huenda zikafunguliwa mwezi Januari mwaka ujao, Wizara ya Elimu imeweka mikakati na sheria zinazopaswa kuzingatiwa kabla kufunguliwa.

Mojawapo, ni kuwa na madarasa na madawati ya kutosha ili kuafikia kigezo cha umbali kati ya mwanafunzi na mwenzake, umbali zaidi ya mita moja na nusu, kati ya matakwa mengine kuzuia msambao wa Covid-19.

Ni mahitaji ambayo wamiliki wa shule za kibinafsi, hata ingawa wanayaunga mkono, wanasema ni ghali kumudu kipindi hiki, wakihoji wanategemea mapato ya shule ilhali zilifungwa Kenya ilipothibitisha kuwa mwenyeji wa virusi vya corona.

Wakiongozwa na Stephen Mathenge, mmiliki wa Shule ya Msingi Kaunti ya Kirinyaga, wameiomba serikali kuwapiga jeki ili kuyahitimisha. “Shule za kibinafsi zimekuwa na mchango mkuu katika sekta ya elimu nchini. Shule na taasisi zote za elimu zilipofungwa kwa sababu ya Covid-19, mianya yetu kupata mapato nayo ilifungika. Ndio, tunaunga mkono mapendekezo ya serikali kuzuia kuenea kwa corona miongoni mwa wanafunzi shuleni, ila kwa sasa baadhi yetu hatuna fedha za kutosha kuafikia kikamilifu mikakati iliyowekwa,” Bw Mathenge ameambia ‘Taifa Leo’ katika mahojiano ya kipekee.

Akitumia mfano wa kuwepo na madarasa na madawati ya kutosha, Mathenge amesema ni hatua ambayo itawagharimu kiasi kikubwa cha pesa, anazosema kwa sasa ni kibarua kuzipata.

“Kwa unyenyekevu, tunaiomba serikali ikiwezekana itujumuishe kwenye orodha ya watakaopewa madawati kupitia mpango uliozinduliwa na Rais,” akasema mmiliki huyo wa shule ya kibinafsi yenye zaidi ya wanafunzi 250.

Kauli ya Bw Mathenge imejiri siku moja baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuzindua mradi wa utengenezaji madawati zaidi ya 650, 000 yanayotarajiwa kusambazwa katika shule za umma, msingi na upili.

Mpango huo umeratibiwa kugharimu kima cha Sh1.9 bilioni, Rais Kenyatta Alhamisi akizungumza katika mtaa wa Umoja, Nairobi, wakati wa uzinduzi huo, akisema mradi huo upo chini ya mpango wa Kazi Mtaani.

Aidha, kiongozi huyo wa nchi alisema uundaji wa madawati hayo utakabidhiwa mafundi wa mbao wa humu nchini, na kwamba unalenga kupiga jeki vijana.

“Mbali na madawati, serikali itupige jeki kuongeza idadi ya madarasa na kuafikia mahitaji mengine muhimu na ya bei ghali. Kwa hakika, shule za kibinafsi nazo zina idadi kubwa ya watoto,” akasema mmiliki wa shule moja ya kibinafsi kiungani mwa jiji la Nairobi.

Baadhi ya shule za kibinafsi tayari zimefungwa kabisa kufuatia mikakati na sheria za ufunguzi wanazodai ni ghali kuafikia.

‘Taifa Leo’ imethibitisha kufungwa kwa Shule ya Kibinafsi ya Brainstone Academy, iliyoko kiungani wa jiji la Nairobi. “Mwezi Agosti tuliarifiwa tuendee chochote tunachomiliki shuleni kwa kuwa haitafunguliwa tena,” Caroline Ng’ang’a mmoja wa walimu katika shule hiyo akasema.

Shule ya Kibinafsi ya Grand Kago, Karatina Kaunti ya Nyeri, wazazi walishauriwa kutafuta shule mbadala kwa kile walifahamishwa kama kufungwa kabisa. “Tuliambiwa ikiwa itaendelea kuhudumu, tutalipa bei ghali. Kwa mfano, wanaolipa karo Sh10, 000 itakuwa mara tatu, Sh30, 000,” akaelezea mzazi mmoja wa shule hiyo.

Ikizingatiwa kuwa shule nyingi za kibinafsi hutumia mabasi kubeba watoto wanapoenda shuleni na kutoka, amri ya kila gari la abiria lisafirishe asilimia 60 ya idadi jumla ya wanaopaswa kubebwa mara moja sharti itekelezwe.