BURUDANI: Msanii anayeinukia ambaye ana ndoto ya kuwa daktari
Na MARGARET MAINA
MSANII Shirleen Vobic, 10, tayari ameshajipatia jina katika kaunti ya Nakuru.
Ana talanta ya uimbaji na amerekodi wimbo wake wa kwanza uitwao ‘Nakuru’ na amesainiwa chini ya Sturnford.
Katika kuwafikia mashabiki amefungua chaneli katika jukwaa la YouTube.
Wimbo wake pia uko kwenye toni za Skiza.
Shirleen ni mwanafunzi wa darasa la tano katika shule ya Excel Grassland Academy ambaye alianza kuimba akiwa shule ya chekechea.
“Bado ninaimba katika kanisa letu na ninakusudia kuendelea kwa neema ya Mungu. Pia katika ushirika wetu wa nyumbani, mimi huongoza wakati wa sifa na ibada,” anasema.
Kilichomshawishi kuimba kuhusu Nakuru ni kuufahamu kuwa ni mji mzuri, safi na kwa sababu aliuona kama taa ya Kenya ambayo inahitajika kuthaminiwa.
Shirleen alituzwa kuwa mwimbaji bora katika Kaunti ya Nakuru katika hafla ya mtindo wa T-shee Fashion House.
“Mama yangu na lebo yangu ya kurekodi wamenisaidia katika kila hatua,” anasema.
Yeye pia anapenda kuogelea na kudensi.
Ingawa ulimwengu wa wasanii umejaa, Shirleen amedhamiria kuwa nyota.
Yeye ana ndoto ya kuwa daktari wa upasuaji na pia kuwasaidia maskini lakini pia chokoraa.
“Ninasawazisha masomo ya shuleni na talanta yangu nikijua kuna wakati wa kila kitu. Aidha nyumbani ninayo ratiba ya kazi ya shule inayosimamiwa na mama yangu na upande wa muziki meneja wangu wa lebo ndiye msimamizi,” anafafanua.
Shirleen anaiga mfano wa mama yake.
“Ningependa kufuata nyayo zake; napenda jinsi anavyompenda Mungu. Yeye ni mpambanaji na mwanamke hodari na amenilea kwa njia ya kipekee,” anasema.
Siri ya kujenga mustakabali wa sanaa endelevu upo katika kuwafanya wasanii wanaoinukia kuwa katika mstari wa mbele leo ima iwe ni katika elimu au mengineyo.
Shirleen anawashauri wasanii wanaoinukia kuwa na ujasiri, watie bidii katika kila zuri walifanyalo.