Seneti yapinga KDF kupewa mamlaka ya kusimamia KMC
Na CHARLES WASONGA
MASENETA wamepinga hatua ya serikali kuhamisha usimamizi wa Kiwanda cha kutayarisha Nyama Nchini (KMC) kutoka Wizara ya Kilimo hadi ile ya Ulinzi wakisema hatua hiyo ni kinyume cha Katiba.
Wakichangia hoja kuhusu suala hilo Alhamisi, walisema hatua hiyo ni haramu kwa sababu uamuzi huo ulifikiwa bila kushirikishwa kwa umma katika mpango huo, ikizingatiwa kuwa KMC ni asasi ya serikali iliyobuniwa kutokana na sheria iliyotungwa na bunge.
Huku wakilaani kile walichotaja kama mwenendo mbaya wa Rais Kenyatta kuweka usimamizi wa asasi za umma chini ya wanajeshi, maseneta hao wamewataka mawaziri Peter Munya (Kilimo) na Monica Juma (Ulinzi) kufika mbele yao kuelezea sababu zilichangia kuhamishwa kwa KMC hadi jeshi (KDF).
“Mheshimiwa Spika mawaziri hao wawili sharti waelezee bunge hili misingi ya kisheria iliyotumika kufanisha kuhamishwa kwa KMC hadi KDF na ni kwa nini umma haukuhusishwa inayohitajika kikatiba,” akasema Seneta wa Machakos Boniface Kabaka akiwasilisha rasmi hoja ya kupinga hatua hiyo.
Seneta wa Narok Ledama Ole Kina alisema kuwa ikiwa Rais Uhuru Kenyatta alihisi kwamba kuna haja ya kuhamishwa kwa kiwanda hicho hadi KDF, angefanya hivyo kupitia bunge. Alisema ni kinaya kuwa KMC inawekwa chini ya usimamizi wa jeshi linalodaiwa Sh7 bilioni.
“Mheshimiwa Spika tumepata habari kuwa KDF ndio inachangia kuporomoka kwa KMC kwa kukosa kulipa deni la zaidi ya Sh7 bilioni inayodaiwa na kiwanda hicho. Mbona tunajaribu kusuluhisha shida kwa kubuni shida nyingi? Nani atalipa deni hilo?” akasema
Naye Seneta wa Isiolo Fatuma Dullo alisema itakuwa vigumu kwa raia kufanya kazi na KDF kutokana na hofu iliyoko miongoni mwa raia dhidi ya wanajeshi.
“Hata ingawa KMC imezongwa na shida ya usimamizi hali ambayo imechangia kupata hasara, suluhu sio kuhamisha na kuiweka chini ya usimamizi wa jeshi. Wafugaji ambao ni wateja wakuu wa KMC watahusika vipi na wanajeshi?” akauliza.
Wengine waliopiga hatua hiyo ni maseneta Abishiro Halake (Seneta Maalum), Ali Wario (Tana River), Abdullahi Ali (Wajir) na Enock Wambua (Kitui).
Hata hivyo, Seneta wa Garissa Yusuf Haji aliunga mkono hatua hiyo akisema jeshi limedhihirisha kuwa linaweza kusimamia vizuri asasi za umma; huku akitoa mfano mwa Meja Jenerali Mohammed Badi anayesimamia majukumu makuu ya kaunti ya Nairobi.
KMC ilhamishwa hadi KDF wiki jana kupitia amri ya Rais Kenyatta. Amri hiyo iliwasilishwa na Waziri Munya kwa Katibu wa Idara ya Uvuvi Harry Kimtai.
“Kufuatia kuhamishwa kwa majukumu ya KMC kwa wizara ya ulinzi kutokana na amri ya Rais, unaagizwa kuhakikisha uhamisho huo umetekelezwa bila changamoto yoyote,” Bw Munya akasema kwenye barua aliyoiandika mnamo Septemba 7, 2020.