Wanaharakati 4 wakamatwa kwenye maandamano
NA FAUSTINE NGILA
Wanaharakati wanne walikamatwa Jumatatu kwenye maandamano ya wakazi wa Nakuru walioitaka serikali kuwanasa waliomumunya pesa za kupigana na janga la corona.
Polisi waliwalaumu wanne hao,Vincent Tanui, John Onyang’o, John Otingo na David Towet kwa kuongoza maandamano kinyume na sheria.
Maandamano hayo yalihusisha mamia ya watu kutoka eneo la Railways kuelekea kwenye afisi ya Kamishna wa Bonde la Ufa George Natembeya.
Polisi walisema kwamba maandamano hayo yalifanyika kinyume na mikakati iliyowekwa na wizara ya afya ya kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona.
Wandamanaji hao walizua vurugu wakitaka kujua jinsi fedha hizo za kupambana na janga la corona zilitumika wakati polisi wa kukabiliana na maandamano waliwasili.
Walibeba mabango yaliokuwa na jumbe tofauti zilizokashifu wizi wa pesa za corona. “Wakamate wezi wa pesa za corona,” waliimba.
Wakiogozwa na Bw David Kuria, waliitaka serikali kutoa taarifa jinsi fedha hizo zilizotolewa zilitumika.
Bw Kuria alikemea kukamatwa kwa wanne hao akisema kwamba ilikuwa kinyume na sheria na kuwa maandamno hayo yalikuwa ya amani.