• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Harusi yasababisha vifo vya watu 7

Harusi yasababisha vifo vya watu 7

Na AFP

HARUSI moja eneo la mashambani la Maine ilichangia maambukizi ya virusi vya corona na kusababisha vifo vya watu saba na wengine 177 wakaambukizwa virusi hivyo.

Kisa hicho kimeibua upya taharuki kuhusu virusi hivyo katika eneo la Kaskazini Mashariki mwa Amerika, lililotumai kwamba lilikuwa limeepukana kabisa na athari zake.

Karamu hiyo ya kufunga ndoa iliyofanyika mapema Agosti ilihudhuriwa na watu 65 huku ikikiuka kiwango rasmi kinachokubalika cha watu 50.

Ibada iliyoandaliwa katika Kanisa la Baptist ilifuatiwa na sherehe katika hoteli ya Big Moose Inn – maeneo yote mawili yakiwa karibu na mji wa kifahari wa Millinocket, wenye idadi ya watu 4,000 pekee.

Siku kumi baadaye, watu kadhaa waliohusishwa na harusi hiyo walipatikana na Covid-19 ambapo Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Maradhi mjini Maine vilianzisha uchunguzi.

Mkurugenzi wa kituo hicho, Nirav Shah, mnamo Alhamisi alitoa takwimu mpya kuhusu hafla hiyo, akiongeza kuwa hakuna yeyote miongoni mwa watu wote saba waliofariki, alikuwa amehudhuria harusi hiyo.

Maafisa wa kufuatilia mtagusano walihusisha harusi hiyo na maeneo kadhaa yenye kiwango cha juu zaidi cha maambukizi ya virusi hivyo nchini humo, ikiwemo visa zaidi ya 80 katika gereza moja iliyo umbali wa kilomita 379, ambayo mlinzi wake mmoja alihudhuria harusi hiyo.

Visa vingine 10 vinavyotuhumiwa vilipatikana katika kanisa moja la Baptist eneo hilo huku maambukizi 39 na vifo vya watu sita vikitokea katika nyumba ya wazee iliyo maili 100 kutoka Millinocket.

Kwa jamii na eneo hilo kwa jumla lililokuwa limelegeza masharti ya kuepuka kutangamana kijamii yaliyoanzishwa mwanzoni mwa janga hilo, ripoti hizo zilikuwa ukumbusho katili.

“Tuliposikia kuhusu mkurupuko huo kila mtu alinyong’onyea mno. Punde baada ya mkurupuko huo kutokea, tulifunga tena kabisa mji huo,” alisema Cody McEwen, mkuu wa baraza la mji huo.

Baadhi ya wakazi walielekeza hasira yao dhidi ya waandalizi wa hafla hiyo ikiwemo hoteli hiyo iliyopokonywa leseni yake kwa muda.

“Sidhani walipaswa kufanya harusi hiyo. Nafikiri walipaswa kuwa na watu wachache jinsi wanavyostahili kuwa. Hatuwezi kwenda popote au kufanya kitu chochote,” alisema Nina Obrikis, mshirika wa kanisa la Baptist ambapo harusi hiyo ilifanyika.

Gavana wa Maine, Janet Mills mnamo Alhamisi alitoa onyo dhidi ya wakazi 1.3 milioni wa eneo hilo.

You can share this post!

Ugaidi wafanya vijiji Lamu visalie mahame

Mbunge wa Thika azimwa kutoa msaada kwa walemavu