• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 12:46 PM
Mbunge wa Thika azimwa kutoa msaada kwa walemavu

Mbunge wa Thika azimwa kutoa msaada kwa walemavu

Na LAWRENCE ONGARO

JUHUDI za mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina kupeana viti vya magurudumu kwa walemavu zilizimwa na watu ambao hakuwataja hadharani.

Mbunge huyo alikuwa amejiandaa kuzuru eneo la Ndumberi, Kaunti ya Kiambu mnamo Ijumaa ili kusambaza viti vya magurudumu kwa walemavu wapatao 300.

Mbunge huyo alisikitika akisema wakati kama huu wa janga la Covid-19 walemavu wanahitaji viti hivyo kwa sababu vitawazuia kutambaa chini na kupata uchafu sakafuni.

“Watu fulani wanataka kuniingiza kwa siasa duni lakini mimi siko huko; azma yangu kuu ni kuona ninatenda kazi ambayo inabarikiwa na Mwenyezi Mungu,” alisema Bw Wainaina.

Alisema wakfu wa ‘Jungle Foundation’ umekuwa ukisaidia wasiojiweza kwa zaidi ya miaka kumi mfululizo na kwa hivyo haoni ni kwa nini mtu ama watu fulani wanamuonea kijicho wakati anawatumikia wananchi kwa moyo mmoja.

Alisema viti hivyo ni vya thamani ya Sh4 milioni na atafanya juhudi kuona ya kwamba walemavu hao wanapokea viti hivyo kwa sababu tayari zimpimwa na kiwango cha kila mmoja.

Alisema wakfu huo unajali wakulima, wagonjwa na wale wanaohitaji misaada popote pale kote nchini.

Alisema baadhi ya maeneo ambazo wamezuru ni Trans Nzoia, Taita Taveta, na hata Baringo ili kuwajali watu wanaohitaji misaada.

Afisa wa kitengo cha afya katika wakfu huo Bi Joyce Njeri alisema lengo lao kuu huwa ni kuwajali walemavu, wasiojiweza kabisa na wazee.

“Mara nyingi sisi huzuru maboma ya wazee na walemavu kuelewa matatizo wanayopitia kabla ya kuwasaidia na vifaa tofauti,” alisema Bi Njeri.

Alisema mara nyingi huwa wanasaidiwa na vyakula, blanketi, na hata viti vya magurudumu.

Alisema mpango wa kuwapatia walemavu viti vya magurudumu ulikuwa ni muhimu kwao lakini inasikitisha kuona ya kwamba sasa walikosa msaada huo.

“Tunajua wengi walijiandaa kupokea viti vya magurudumu lakini sasa inamaanisha wataendelea kupata shida zao za kila siku. Hata hivyo bado tutajaribu tuwezavyo kuwafikia kwa vyovyote vile,” alisema Bi Njeri.

Mlemavu kutoka Thika Bw Simon Ngugi aliyetarajia kupata kiti chake bila mafanikio alisema yule amewakatia matumaini yao ni mtu asiye na utu kabisa.

“Sisi kama walemavu hatungetaka siasa ziingiizwe katikati yetu kwa manufaa ya watu wachache. Wakati huu wa corona ndiyo tunataka msaada zaidi na kwa hivyo tunataka viti hivyo vya magurudumu ili tuweze kujisafirisha wenyewe popote pale,” alisema Bw Ngugi.

  • Tags

You can share this post!

Harusi yasababisha vifo vya watu 7

Hakuna vifo vya corona Jumamosi