Habari Mseto

AIBU PUMWANI: NMS yaomba msamaha

September 19th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

IDARA ya Huduma za Jiji la Nairobi (NMS) imeomba msamaha kwa umma, na haswa akina mama, kufuatia kisa ambapo mama mmoja alidaiwa kujifungua nje ya Hospitali ya Kujifungulia akina Mama ya Pwani baada ya kutelekezwa.

Kwenye taarifa Jumamosi Mkurugenzi wa Huduma za Afya katika NMS Josphine Kibaru Mbae alisema kisa hicho cha kusikitisha kilitokea wakati wahudumu wa hospitali hiyo walisusia kazi.

“Hata hivyo, tunachukua fursa hii kuomba msamaha kwa Wakenya wote na hususan akina mama wetu kwa tukio kama hili la kusikitisha,” Bw Mbae akasema.

Alithibitisha kuwa kisa hicho kilitokea mnamo Septemba 13, 2020.

Video kuhusu kisa hicho ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii na kuibua kero kutoka kwa wananchi, akiwemo Mbunge Mwakilishi wa Nairobi Esther Passaris.

Bi Mbae alisema hii ilikuwa ni siku mbili baada ya wauguzi kuanza mgomo wao ambao ulifikia kikomo baada ya NMS na wahudumu wa afya kukubaliana kuhusu masharti ya kuzingatia kurejea kazini.

“Walinzi walimzuia mama huyo kuingia ndani ya majengo ya hospitali. Hata hivyo, muuguzi ambaye alikuwa katika zamu alifahamisha kuhusu kisa hicho na akakimbia hadi eneo la tukio na kumsaidia mama huyo,” akaongeza Bi Mbae.

Alisema NMS inamshukuru muuguzi huyo kwa kumsaidia mama huyo ambaye pamoja na mwanawe sasa wako salama na waliruhusiwa kwenda nyumbani mnamo Ijumaa Septemba 18, 2020.

Bi Mbae alisema kuanzia sasa NMS itawapa mafunzo maalum maafisa wa kuwapokea wageni katika hospitali zake zote pamoja na afisi zingine za kutoa huduma muhimu “ili kuzuia tukio la aibu kama hilo lililotokea katika Hospitali ya Pwani.”

“Hata hivyo, ningependa kuwahakikishia Wakenya kuwa mlinzi aliyemzuia mama huyo mja mzito kuingia hospitali amechukuliwa hatua za kinidhamu. Aidha, kitengo cha kuwahudumia wateja kimeanzishwa katika hospitali hiyo,” mkurugenzi huyo akaeleza.

Bi Mbae alisema kuanzia sasa maafisa wa polisi ndio watakuwa wakitoa ulinzia katika Hospitali hiyo, Hospitali ya Mama Lucy. Hospitali ya Mbagathi, Hospitali ya Mutuini na ile ya Dagoreti ili kuimarisha utoaji huduma.