• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 5:55 AM
Rais anavyozua taharuki kuhusu hatima yake ya kisiasa

Rais anavyozua taharuki kuhusu hatima yake ya kisiasa

Na BENSON MATHEKA

Kauli za baadhi ya viongozi na wanasiasa kwamba Rais Uhuru Kenyatta atakuwa na nafasi ya kubaki uongozini katiba ikirekebishwa kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI) alioanzisha baada ya handisheki yake na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga, zinaweza kubadilisha siasa za nchi hii.

Wadadisi wanasema kuwa Rais Kenyatta mwenyewe amekuwa akichanganya Wakenya kuhusu msimamo wake kwa suala hili asionekane kwamba anataka kukwamilia mamlakani.

Akiwa Nyeri 2018, wakati madai kwamba angali na umri mdogo usiomfaa kustaafu katika siasa yalipoibuka, Rais Kenyatta alisema hatajali iwapo katiba itakayofanyiwa mageuzi na nyadhifa mpya za Waziri Mkuu kubuniwa itamruhusu kuhudumu.

Kulingana na Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya wafanyakazi nchini (Cotu), ambaye alikuwa wa kwanza kudokeza kwamba Unuru hatastaafu siasa 2022, katiba ikirekebishwa na nafasi zaidi kubuniwa, hakuna kitakachomzuia Rais Kenyatta kugombea uongozi tena.

Juma moja lililopita, Rais Kenyatta aliambia wakazi wa Ruaka, Kiambu kwamba yuko tayari kustaafu kipindi chake kitakapokamilika hata kama angali na nguvu za kuendelea kuhudumu.Wadadisi wanasema kwamba hatua yoyote ambayo Rais Kenyatta atachukua, itategemea matokeo ya kura ya maamuzi iwapo itafanyika.

“Kuna lililo moyoni mwake nalo ni kuweka mazingira ya kikatiba kwanza ya kuhakikisha hatua yoyote atakayochukua haitazidisha uhasama na chuki za kisiasa nchini. Hii ndiyo sababu amekuwa akisema kwamba lengo la BBI ni kuunganisha Wakenya,” asema mdadisi wa siasa Geoffrey Kamwanah.

Kwa sasa, anaeleza, katiba inamruhusu kustaafu 2022 na kwa kutaka irekebishwe miaka miwili kabla ya uchaguzi na kauli za Bw Atwoli na wenzake kwamba wanapanga aendelee kuhudumu, ni ishara hana nia ya kustaafu,” asema.

Wachanganuzi wa siasa wanasema Rais anayetaka kuongeza muda wake uongozini hasemi wazi kwamba anataka kufanya hivyo.

“Huwa wanatumia vibaraka wao kushinikiza mabadiliko ya kikatiba na kisheria. Yakifaulu, wanayatumia kugombea. Hii imefanyika katika nchi tofauti ulimwenguni na hasa kusini mwa jangwa la Sahara. Sidhani hili ndilo lengo la Rais Kenyatta lakini Wakenya wakimruhusu sio rahisi kukataa,” asema.

Lakini kulingana na mdadisi wa siasa John Kilimo, mazingira ya siasa Kenya ni tofauti na nchi nyingine na huenda Wakenya wasikubali marekebisho ya katiba ya kuongeza muda wa rais au kumruhusu kushikilia wadhifa mwingine ukibuniwa kupitia referenda.

“Kwanza, kuna vigogo wengi wa kisiasa kutoka maeneo tofauti wanaomezea mate urais akiwemo Naibu Rais William Ruto na Bw Odinga. Tayari kuna madai kwamba Uhuru analenga kumsaliti Ruto kwa kukataa kumuunga mkono kumrithi. Ruto na washirika wake wametangaza hawarudi nyuma,” asema Koech.

“Kwa upande mwingine, Bw Odinga na washirika wake wameanza kujiandaa kwa safari ya Ikulu. Wawili hawa wana wafuasi wengi na hivyo basi, kwa Rais Kenyatta kuongeza muda wa kuhudumu kwa vyovyote vile, kunaweza kutumbukiza nchi katika matatizo makubwa ya kisiasa Ruto na Raila na viongozi wengine wakihisi kusalitiwa,” asema Bw Koech.

Kulingana na Bw Kamwanah, mwanya ambao Rais Kenyatta anaweza kutumia kubaki katika uongozi ni kupitia wadhifa wa waziri mkuu akimsaidia Bw Odinga kushinda urais.

“Nafikiri huu ndio mpango wao. Wapanue nyadhifa za uongozi kupitia BBI ili wawashirikishe vigogo wengine wa kisiasa. Tatizo ni kuwa iwapo Uhuru atakuwa waziri mkuu punde tu baada ya kuhudumu vipindi viwili kama rais, atakayekuwa rais hatakuwa na nguvu,” asema Bw Kamwanah.

Japo Bw Odinga amekuwa akipuuza madai ya Dkt Ruto na wandani wake kwanba BBI inalenga kubuni nyadhifa za uongozi kutimiza maslahi ya watu wachache, ripoti ya BBI ilipendekeza mfumo wa serikali ulio na Rais, waziri mkuu na manaibu wawili.

Akiwa Mombasa wiki jana, Bw Odinga alisema keki ni ndogo na inafaa kuongezwa ili kila sehemu ya Kenya ipate kipande. Alisema kwamba aliyokubaliana na Rais Kenyatta kwenye handisheki yao ni zaidi ya nyadhifa za uongozi.

Duru zinasema kwamba kuna mpango wa vigogo wa kisiasa kutoka maeneo tofauti kuungana kubuni muungano mkubwa wa kisiasa kuhakikisha BBI itafaulu nyadhifa zaidi za uongozi zibuniwe. Hii ikifanyika, vigogo hao, watagawana nyadhifa hizo ili kila sehemu iwakilishwe serikalini.

“Hapa ndipo Rais Kenyatta atapata nafasi ya kuhudumu serikalini akiwakilisha Mlima Kenya. Ataweza kugombea urais iwapo marekebisho ya katiba yatatoa mwanya kufanya hivyo au awe waziri mkuu mwenye mamlaka. Kwa kufanya hivi, vigogo wa siasa hawatalalamika. Yote itategemea matokeo ya kura ya maamuzi,” asema Bw Kamwanah.

Anasema hii inaweza kuwa sababu ya Rais Kenyatta kujivuta kuteua mrithi wake katika eneo la Mlima Kenya. Lakini Bw Peter Ouma, mdadisi wa siasa na mtaalamu wa masuala ya uongozi anasema kwamba huenda Rais Kenyatta binafsi anataka kuacha Kenya ikiwa imeungana akistaafu.

“Kauli kwamba anataka kuendelea kutawala kwa sasa hazina msingi kwa sababu amesema hataki kuona Wakenya wakimwaga damu kila baada ya miaka mitano. Hata hivyo, haikosi kuna watu wanaotaka asibanduke ili waendelee kufurahia matunda ya utawala wake,” asema.

Bw Ouma anasema kwa sasa, ishara ni kwamba Bw Odinga ambaye ni mshirika wa Rais katika handisheki atagombea urais. “Kwa Rais Kenyatta kuamua kubadilisha katiba ili apate nafasi ya kuendelea kutawala ni kutumbukiza Kenya katika orodha ya nchi ambazo viongozi hukwamilia mamlakani,” asema.

You can share this post!

ONGAJI: Nani ataokoa maisha ya vijana?

Kizungumkuti cha Mukhisa Kituyi katika uchaguzi wa 2022