Habari

Sonko aelekea korti ya rufaa kuhusu usimamizi wa jiji

September 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na JOSEPH WANGUI

GAVANA wa Nairobi, Bw Mike Sonko ameelekea katika mahakama ya rufaa kulalamikia uamuzi wa Mahakama Kuu uliohalalisha Idara ya Huduma za Nairobi (NMS).

Kwenye notisi ya rufaa aliyowasilisha kupitia kwa kampuni ya uwakili ya Kurauka & Company, gavana huyo alisema hakuridhishwa na uamuzi wa Jaji Hellen Wasilwa wa Mahakama ya Ajira na Leba, uliotolewa Septemba 17.

Gavana Sonko tayari amemkabidhi Mkuu wa Sheria nakala ya notisi ya kumfahamisha kuhusu hatua yake ya kutaka kukata rufaa.

Hatua hiyo ya Bw Sonko ni ishara kwamba, mvutano kuhusu udhibiti wa jiji la Nairobi baina ya Rais Uhuru Kenyatta na Gavana Sonko haujafikia kikomo.

Mahakama ya Leba ilibatilisha uamuzi wake wa awali kuwa NMS inayoongozwa na Meja Jenerali Mohammed Badi, ilibuniwa kinyume cha katiba.

Gavana Sonko pia amekosoa uamuzi wa Jaji Wasilwa kuwa kuhamishwa kwa wafanyakazi 6,052 kutoka Kaunti ya Nairobi hadi kwa NMS kulikiuka katiba.

Jaji alitupilia mbali ombi la Gavana Sonko kutaka kurudishiwa wafanyakazi wa kaunti kutokana na kigezo kwamba hakushauriwa.

Awali, Jaji Wasilwa alikuwa ameamua kuwa baadhi ya majukumu yalihamishwa kutoka serikali ya Kaunti ya Nairobi hadi serikali kuu bila kuhusisha madiwani na maafisa wengine wa kaunti.

Lakini katika uamuzi wake wa hivi majuzi, Jaji Wasilwa alibatilisha uamuzi wa awali na kusema kuwa, shughuli hizo zilihamishwa kwa kuzingatia katiba.

Alisema ushahidi aliopata kutoka kwa bodi ya PSC, NMS na Mkuu wa Sheria ulionyesha kuwa Bunge la Kaunti ya Nairobi lilihusishwa.

Alizingatia barua iliyoandikwa na Mkuu wa Sheria ikifahamisha Bunge la Kaunti ya Nairobi kuhusu uamuzi wa kuhamisha baadhi ya majukumu kutoka kwa serikali ya Gavana Sonko hadi Serikali Kuu.

Jaji pia alisema kuwa aliridhika na ushahidi kuwa kulikuwa na vikao vya kupokea maoni kutoka kwa wakazi wa Nairobi katika kaunti ndogo zote 17.

Rekodi za mazungumzo ndani ya bunge la kaunti pia zilionyesha kuwa madiwani walijadili suala la kuhamisha mamlaka.

“Nimetathmini stakabadhi zilizoambatishwa na nilibaini kuwa Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi mnamo Februari 27, 2020, alifahamisha madiwani kuhusu uamuzi wa kuhamisha shughuli nne kwa Serikali ya Kitaifa. Aidha, bunge la kaunti lilibuni kamati maalumu kushughulikia suala hilo,” akasema Jaji.