• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:50 AM
Wabunge waapa kushinikiza NG-CDF iongezwe

Wabunge waapa kushinikiza NG-CDF iongezwe

Na GEORGE SAYAGIE

WABUNGE wameapa kuwasilisha hoja itakayoishinikiza Serikali ya Kitaifa kuongeza kiwango cha fedha za Hazina ya Kustawisha Maeneobunge (NG-CDF) kutoka asilimia 2.5 hadi asilimia tano ya bajeti ya taifa.

Kauli hiyo ilitolewa na wabunge watatu Jumamosi, walipofanya ziara maalum kuhusu utekelezaji wa hazina hiyo katika Kaunti Ndogo ya Narok Magharibi.

Wabunge hao, ambao ni wanachama wa Kamati ya Bunge Kuhusu Hazina ya NG-CDF, walisema hazina hiyo imeleta maendeleo makubwa katika maeneo ya mashinani.

“Tunawaomba Wakenya kutuunga mkono kwenye juhudi zetu kuishinikiza serikali kuongeza kiwango cha fedha inazotoa kwa hazina ya CDF, kwani manufaa yake yameonekana kote nchini,” akasema mwenyekiti wa kamati hiyo, Bw Wafula Wamunyinyi.

Bw Wamunyinyi, ambaye pia ni mbunge wa Kanduyi, alisema kuwa watapitisha sheria kuongeza mgao wa fedha hizo ili kuwawezesha wabunge kutekeleza miradi zaidi. Alisema Sh50 bilioni ambazo ziliongezwa kwenye hazina hiyo hazitoshi, ila kiwango hicho kinapaswa kuongezwa hadi asilimia tano ya bajeti.

Mwenyekiti huyo alilisifia eneobunge hilo kwa kuwekeza kwenye sekta ya elimu.

Alisema kwamba kamati imejitolea kuhakikisha fedha hizo zimetumiwa vizuri na wabunge wamemaliza miradi waliyoianza. Alieleza kuwa kwa hilo, wabunge wanapaswa kuruhusiwa kuendelea kusimamia hazina hiyo.

Mbunge wa Bahati, Kimani Ngunjiri, ambaye pia ni mwanachama wa kamati, aliunga mkono wito huo, akisema kiwango cha sasa hakitoshi.

“Tunataka kuhakikisha kwamba fedha nyingi zimeelekezwa kwenye hazina hiyo kutoka asilimia 2.5 ya bajeti. Hili litawawezesha wabunge kuendeleza miradi zaidi ya maendeleo katika maeneobunge yao,” akasema Bw Ngunjiri, baada ya kuzuru shule za msingi za Kisheimoruak na Sikinani.

Mbunge alisema kuwa hazina hiyo ndiyo mradi pekee wa kitaifa ambao umeibukia kuistawisha nchi kimaendeleo tangu uhuru. Hata hivyo, kamati ilieleza kwamba huenda baadhi ya wanafunzi wakashindwa kufika shuleni baada ya shule kufunguliwa upya kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika eneo hilo.

Mbunge wa Narok Magharibi, Gabriel Tongoyo alisema hazina hiyo imeimarisha maendeleo kwa kiwango kikubwa katika eneo hilo, japo akalalamikia hali mbaya ya barabara zinazounganisha taasisi mbalimbali.

Hivyo, aliirai serikali kutoa fedha kuyastawisha maeneo kame ili kuwawezesha wabunge kuwekeza zaidi kwenye miradi ya maendeleo.

Mwito huo unajiri siku chache baada ya migawanyiko mikali kuibuka Seneti kuhusu mfumo wa ugavi wa fedha za kaunti.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Pesa za umma zitumiwe vyema

Polisi watibua kikao cha Khalwale kwa ‘amri kutoka juu’