Uhuru kuhutubia mkutano wa UNGA Jumanne kupitia mtandao
Na CHARLES WASONGA
RAIS Uhuru Kenyatta atahudhuria na kuhutubia Kongamano Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) kwa njia ya mtandao kutoka Nairobi.
Hata hivyo, Kenya itawakilishwa moja kwa moja katika mkutano huo na maafisa wa ubalozi wa Kenya jijini New York wakiongozwa na balozi Lazarus Amayo.
Mkutano huo ambao unaanza Jumanne, Septemba 22, 2020, unatarajiwa kukamilika mnamo Septemba 29.
“Uendeshaji na taratibu za Kongamano la 75 la UNGA hasa sehemu za viongozi wakuu zitakuwa za kipekee kutokana hofu ya janga la Covid-19. Kwa mara ya kwanza katika historia ya UNGA vikao vingi vitaendeshwa kwa njia ya mtandao,” taarifa kutoka Wizara ya Masuala ya Kigeni ilisema.
Katika hali ya kawaida marais na viongozi wengine wa ulimwengu hukongamana kila mwaka katika makao makuu ya UNGA jijini New York kutoa hotuba kuhusu mada mbalimbali kupitia jukwaa kuu.
Ajenda kuu zitakazowasilishwa na Kenya katika vikao vya kongamano la mwaka huu 2020 zinajumuisha; amani na usalama, mabadiliko ya tabianchi, mipango ya kuinua hali ya vijana na wanawake, mzigo wa madeni kwa mataifa yanayoendelea na maendeleo endelevu.
Kauli mbiu ya kongamano la mwaka 2020 ni; “Mustakabali tunaotaka, Umoja wa Mataifa tunaotaka; Kuthibitisha kujitolea kwetu kupalilia ushirikiano”.