Ajali ya treni yasababisha msongamano Mombasa
Na WINNIE ATIENO
SERIKALI Jumapili iliwatuma wanajeshi katika eneo la mkasa wa garimoshi la kubeba mafuta ya petroli mjini Mombasa, huku abiria kati ya Nairobi na Mombasa wakitatizika mchana kutwa.
Katibu katika Wizara ya Uchukuzi anayehusika na Uchukuzi wa Baharini, Bi Nancy Karigithu, alisema wanajeshi wa majini (Kenya Navy) walitumwa kuwasaidia polisi kudhibiti hali katika eneo hilo la Kibarani.
“Tumewatuma wanajeshi kudhibiti usalama eneo la ajali na pia katika lango la kuingia na kutoka bandarini. Hili ni eneo la kimataifa na lazima lilindwe ipasavyo,” alisema Bi Karigithu.
Mabogi matano yaliyokuwa yamebeba lita 3,000 za petroli yalianguka na kumwaga mafuta hayo katika eneo la ardhi juu ya bahari, linalounganisha kisiwa na Mombasa na upande wa nchi kavu kwenye barabara ya kuelekea Nairobi.
Tukienda mitamboni, kulikuwa na msongamano mkubwa wa wasafiri, baada ya maafisa wa usalama kuifunga barabara ili kuzuia petroli hiyo kulipuka.
Abiria waliokuwa wakisafiri kati ya Nairobi na Mombasa walilazimika kutumia barabara ya Mazeras – Kalokeni -Mavuweni – Mtwapa – Mombasa.
Ni abiria wa shirika la garimoshi la kisasa (SGR) na wanaotumia uwanja wa kimataifa wa ndege wa Moi pekee walioruhusiwa kupitia lango la Halmashauri ya Bandari (KPA).
Abiria walihitajika kuonyesha ushahidi wa tikiti za usafiri kabla ya kuruhusiwa kutumia njia hiyo, huku wakisindikizwa na maafisa wa usalama.
Kamanda wa polisi wa Mombasa, Bw Johnston Ipara alisema maafisa wake wanachunguza ajali hiyo, ambapo garimoshi hilo lililokuwa limebeba lita 250,000 za petroli liliangusha mabogi matano yaliyokuwa na lita 3,000.
Alisema barabara hiyo itafunguliwa pindi hatari ya mafuta kulipuka itakapokabiliwa. “Tumesimamisha usafiri katika barabara kuu ya Mombasa kuelekea Naiorbi katika eneo la Kibarani sababu ya ajali hii.”
Uchunguzi umeanzishwa kubainisha kiini cha ajali hii,” akasema Bw Ipara alipoenda kudadisi ajali hiyo eneo la Kibarani.
Ajali hiyo ilisababisha uhaba mkubwa wa chakula katika soko la Kongowea. Vyakula kama mboga, matunda, nafaka, samaki husafirishwa kutoka bara kupitia barabara hiyo kuu.
“Nimeamua kuiza vyakula vyangu hapa Changamwe manake kufika Kongowea ni balaa,” akasema George Gathenge mfanyibiashara. Abiria walitakiwa kutumia njia mbadala ikiwemo ile ya Kaloleni, Mavueni, Mtwapa ili kufika Mombasa.