Habari

Maraga azua sokomoko

September 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

USHAURI wa Jaji Mkuu David Maraga kwa Rais Uhuru Kenyatta kuwa anapasa kuvunja Bunge la Taifa na Seneti limezua hali ya kuchanganyikiwa baina ya Wakenya.

Kulingana na Bw Maraga, Katiba imeweka wazi kuwa inastahili Bunge livunjwe na uchaguzi mpya wa wabunge kufanyika iwapo watashindwa kupata mfumo wa kuhakikisha kuwa zaidi thuluthi mbili ya watu waliochaguliwa sio wa jinsia moja.

Mawakili, wabunge, vingozi wa vyama, wanaharakati na wananchi walitoa kauli kinzani, baadhi wakiunga mkono Jaji Maraga na wengine wakimpinga.

Baadhi ya waliounga mkono Jaji Maraga walisema hii ni fursa muhimu kwa Rais Kenyatta kuonyesha Wakenya na dunia nzima kuwa anaheshimu Katiba aliyoapa kulinda na kutii.

Rais wa Chama cha Mawakili Nelson Havi anasema iwapo Rais Kenyatta atapuuza ushauri wa Bw Maraga, sheria zote zinazopitishwa na bunge kuanzia sasa, ama ripoti zake zitakuwa bure.

Bw Havi anasema mishahara ya wabunge pia inapasa kusimamishwa kwani wamo ofisini kinyume cha sheria.

Kiongozi wa Narc-Kenya Martha Karua kwa upande wake alisema hii ni fursa kwa Rais Kenyatta kuonyesha heshima yake kwa Katiba.

“Hakuna vijisababu vyovyote kwa Rais. Ni lazima avunje Bunge la sivyo aweke historia kama Rais aliyevuruga Katiba,” akasema Bi Karua.

“Rais anapaswa kwanza kutii na kutekeleza Katiba. Kwa muda mrefu amekataa kwa ujeuri kutii Katiba inayolenga kuhakikisha jamii yenye usawa,” akasema mwanaharakati Ndung’u Wainaina.

Mwingine aliyeunga mkono kuvunjwa kwa Bunge na Seneti ni Seneta Kipchumba Murkomen wa Elgeyo Marakwet, aliyesema hii ni fursa njema kwa Rais kuwatuma wabunge nyumbani.

Kulingana na Bw Murkomen, Bunge likivunjwa, watakaochaguliwa upya watahudumu kwa miaka mitano na uchaguzi wa 2022 utakuwa wa kuchagua rais, magavana na madiwani pekee.

Lakini kwa upande wake, Wakili Charles Kanjama anasema uchaguzi ambao utaandaliwa iwapo Bunge litavunjwa utakuwa kama uchaguzi mdogo na washindi watahudumu hadi 2022 wakati uchaguzi mpya utakapofanyika.

Kwa upande mwingine kuna wale ambao wanashauri Rais Kenyatta kuchukua hatua zingine kuepusha kile wanasema ni mgogoro wa kikatiba.

Wakili Ahmednassir Abdullahi anasema rais anaweza kupuuza ushauri wa Maraga ama wabunge waende mahakamani kupinga kuvunjwa kwa Bunge.

Kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi anasema japo pendekezo la Bw Maraga ni halali, hilo sio suluhu kwa tatizo la kutopitishwa kwa sheria kuhusu usawa wa kijinsia.

“Kuvunjwa kwa bunge wakati huu kutalemaza mipango yote ya serikali kando na kusababisha mgororo wa kikatiba. Sheria na Katiba zinapasa kutekelezwa kwa njia inayomsaidia mwananchi sio kumuumiza,” akasema Bw Mudavadi.

Alisema muhula wa Bunge umewekwa kuwa miaka mitano, na hivyo kuvunjwa kwake kunamaanisha kuwa muhula wa wabunge watakaochaguliwa utagongana na muhula wa rais na serikali za kaunti.

Kwa upande wake, Tume ya Huduma za Bunge (PSC) ilitaja ushauri wa Bw Maraga kama wenye nia mbaya.

Spika Justin Bw Muturi alisema hatua ya Bw Maraga inaadhibu Bunge la 12 kwa kosa ambalo lililotekelezwa na bunge 11, ingawa hata wakati huo ndiye aliyekuwa spika

Bw Maraga alitoa ushauri wake kwa rais baada ya mabunge hayo mawili kushindwa kupitisha sheria kuhusu jinsia mara nne.

Baadhi ya mawakili walisema kuwa ushauri wa Bw Maraga pia ni tisho kwa BBI kwani iwapo Bunge litavunjwa mchakato huo utakuwa umegonga mwamba.

Wadadisi nao wanasema wabunge na maseneta wanapinga hatua iliyochukuliwa na Bw Maraga kwa hofu kwamba wengi wao hawatachaguliwa tena katika uchaguzi mdogo.

“Imekuwa ada kwamba katika kila uchaguzi mkuu, zaidi ya asilimia 75 ya wabunge hupoteza viti vyao. Miongoni mwa asilimia 25 ambao hufaulu kuhifadhi viti vyao, baadhi yao hutumia njia za mkato,” akasema Bw Martin Andati.

Mchanganuzi huyu wa masuala ya kisiasa anaongeza kuwa wabunge wengi pia wanaogopa gharama ya uchaguzi mdogo ikizingatiwa kuwa baadhi yao wangali wanalipa fedha walizokopa kufadhili kampeni za uchaguzi mkuu wa 2017.