Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nadharia tumizi ya uakifishaji katika lugha ya Kiswahili

September 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MARY WANGARI

MWANAISIMU Leech (1983) akifafanua Nadharia Tumizi ya Uakifishaji iliyoasisiwa na Meyer (1989), anasema kuwa lugha huchunguzwa na kubainishwa kwa kuzingatia viambajengo vinne vikuu.

Kulingana na Leech, viambajengo hivyo vya lugha vimeainishwa katika aina na safu anuwai ambavyo ni pamoja na: maneno, virai au vikundi, vishazi, sentensi, virai au vikundi.

Viambajengo vya lugha huainishwa katika aina mbalimbali ambavyo ni kama zifuatazo:

Maneno – Maneno yameainishwa katika aina mbalimbali ambazo zinajumuisha nomino, vielezi, vivumishi na kadhalika.

Virai – Aina ya virai ni pamoja na kirai kitenzi au kirai kielezi.

Vishazi – Vishazi vinajumuisha aina mbalimbali kama vile kishazi huru, kishazi si huru, kishazi ukomo, kishazi siukomo, kishazi bebwa na kishazi si bebwa.

Jinsi anavyohoji Leech, ili mawasiliano yafanyike kwa njia madhubuti, ni sharti mtumiaji wa lugha yoyote ule awe na ufahamu wa kutosha kuhusu safu na aina ya vipashio vya lugha husika.

Na si katika mawasiliano tu bali katika maandishi vilevile maadam kulingana na mtaalam huyo, kitendo cha kuandika ni matumizi ya lugha katika mawasiliano kimaandishi.

Kwa mantiki hiyo, anahoji kuwa ili sanaa ya uandishi ifanikishwe inavyofaa na kwa ufasaha, ni sharti mwandishi awe na ufahamu kuhusu uakifishaji sahihi ikiwemo matumizi ya alama anuai za uakifishaji.

Hoja hiyo ya Leech ndiyo iliyomchochea Meyer (1989) kuasisi Nadharia Tumizi ya Uakifishaji.

Nadharia Tumizi ya Uakifishaji – Cha msingi kuhusu nadharia hii ni kuhusu umuhimu wa dhima ya viakifishi katika kufanikisha mawasiliano kufanyika.

Azma kuu ya kutumia viakifishi katika maandishi ni kuhakikisha kuwa hadhira lengwa au msomaji anaelewa upesi matini anayosoma pamoja na ujumbe uliokusudiwa kupitishwa na mwandishi.

Viakifishi hutekeleza dhima muhimu ya kutenganisha na kuunganisha vipashio mbalimbali vya lughaview ni vya kisemantiki, kisintaksia au kiprosodi.

Meyer anasisitiza kuwa uakifishaji una mchangamano mkubwa wa kimahusiano na sintaksia, semantiki na prosodi.

Anafafanua kuwa sheria zinafafanua bayana sehemu zinazopaswa kuakifishwa na aina ya viakifishi vinavyopaswa kutumika.

Kanuni hizo za kisarufi zinahusu uteuzi wa viakifishi ambavyo ni mwafaka zaidi katika muktadha husika. Aidha, nadharia tumizi ya uakifishaji imeainisha kanuni na sheria za uakifishaji katika vitengo maalum.

[email protected]

Marejeo

Leech, G. (1983). Principles of Pragmatics. London: Longman.

Stephano, R. (2015). “Uzingatizi wa Viakifishi katika Uandishi wa Kitaaluma: Mifano kutoka Shule za Msingi Tanzania.” Tasnifu ya Shahada ya Uzamivu ya Chuo Kikuu cha Dodoma.