• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 3:04 PM
Viongozi washauriwa kuwajali wananchi kwanza

Viongozi washauriwa kuwajali wananchi kwanza

Na LAWRENCE ONGARO

VIONGOZI wamehimizwa kuweka zingatio katika kuwatumikia wananchi badala ya kupiga siasa za 2022.

Mbunge wa Thika Patrick ‘Jungle’ Wainaina, aliwasuta viongozi ambao ajenda yao kuu ni kuzima maendeleo yanayoletwa na wapinzani wao.

“Mimi kama mbunge wa Thika lengo langu kwa sasa ni kuwatumikia wananchi na halitazimwa na yeyote yule. Nitahakikisha ajenda zangu zote za kuletea wananchi maendeleo zinatimia,” alisema Bw Wainaina.

Ninataka wananchi wawe chonjo na viongozi ambao lengo lao ni kuzima wengine badala ya kujituma na kuendeleza kile kimeanzishwa cha maendeleo.

Aliyasema hayo mnamo Jumanne katika afisi ya NG-CDF mjini Thika alipoangazia jinsi alivyozimwa na viongozi fulani ili asiwape walemavu viti vya magurudumu hivi majuzi.

“Mimi sina wakati wa mashindano na yeyote kwa sababu raha yangu kwa wananchi ni kuona ya kwamba wanafurahia maendeleo,” alisema.

Aliwashauri viongozi popote walipo wawe watu wa kunyenyekea wala sio kuwa na kiburi.

Siasa za Kaunti ya Kiambu zinaonekana zinazidi kupamba moto huku wengi wa viongozi wakijipanga kuwania viti tofauti vya uongozi.

Kiti kinacholeta joto kali kweli ni kile cha ugavana ambapo mirengo tofauti imeanza kuonekana ikijipanga kwa kinyang’anyiro cha mwaka 2022.

Viongozi wanajaribu kutumia mbinu zote wanazoweza kuona ya kwamba mwananchi wa kawaida anaona kile anachotendewa mashinani.

Bw Wainaina aliwashauri viongozi wajifunze kuwa watu wa kujinyima na kutumikia wananchi badala ya kujihusisha na siasa za kukatana miguu.

“Iwapo tutaweza kuhakikisha mwananchi wa kawaida anapata unga mezani kila siku, bila shaka Mungu aliye juu ndiye ataamua kiongozi halisi ni yupi,” alisema mbunge huyo.

  • Tags

You can share this post!

Mudavadi atakuwa debeni 2022 – ANC yasisitiza

LISHE: Jinsi ya kuandaa ‘chickpea curry’